|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA MALIASILI NA MAZINGIRA:MISITU:a) Misitu ya Hifadhi Mkoa una eneo la ardhi lenye ukubwa wa Hekta 7,526,400 na una eneo la misitu iliyohifadhiwa kisheria kiasi cha Hekta 3,340,000 sawa na asilimia 44 ya eneo lote la Mkoa. Eneo lenye misitu katika maeneo ya wazi ni hekta 2,792,100 sawa na asilimia 37 ya eneo lote la Mkoa. Sehemu kubwa ya misitu iko katika Wilaya za Sikonge, Urambo na Uyui. Mazao makuu ya misitu ni mbao, nguzo kwa ajili ya majengo, mkaa, madawa, asali na nta. b) Utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Upandaji Miti: Upandaji Miti hufanywa na watu binafsi, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali katika Vijiji vyote 489 Mkoani na Mijini. Katika Msimu wa 2009/2010 miti ambayo imeshapandwa ni 5,250,010 ambayo ni asilimia 60 ya lengo la kila mwaka la Mkoa la kupanda miti 9,000,000. Wananchi wameshaelimishwa kuhusu Waraka wa Waziri Mkuu Na.1 wa 2009 unaobadilisha siku ya taifa ya upandaji miti kutoka Januari Mosi kwenda Aprili Mosi. c) Utunzaji wa Uoto wa Asili wa Malisho ya Watu binafsi: Watu binafsi Vijijini wametenga jumla ya Hekta, 114,143.7 (Nzega Ha. 11,322, Igunga Ha.6,285, Urambo Ha.829.7, Uyui Ha.38,200, Sikonge Ha.4,971 na Tabora Ha.52,536) kwa ajili ya Malisho na Uoto wa Asili (Ngitiri). WANYAMAPORI@Mkoa una Mapori ya Wanyama yenye Ha. 5,670,966 (Igunga Ha. 110,000, Uyui Ha 966, Urambo Ha.1,750,000, Sikonge Ha. 3,800,000 na Tabora Ha. 10,000) ambayo hutumiwa kwa shughuli za utalii na uwindaji wa Wenyeji. Changamoto kubwa ni kudhibiti Uwindaji haramu unaofanywa na Majangili. Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU) Kanda ya Magharibi kwa kushirikiana na Wananchi kinaidhibiti hali hii kwa kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani majangili wanaokamatwa wakiwa na nyara mbalimbali, Meno ya Tembo na vifaa vya kuwindia, ikiwa ni pamoja na bunduki na risasi. Watuhumiwa huhukumiwa kifungo au faini au vyote viwili kwa mujibu wa sheria.
Ufugaji Nyuki:Ufugaji wa nyuki ni shughuli ya kijadi Mkoani kote ambayo hufanyika katika Misitu na Pori la Akiba la Ugalla kwa utaratibu maalum. Shughuli hii huwaingizia wananchi kipato kutokana na uzalishaji wa Asali na Nta. Katika mwaka 2007/08 wafugaji Mkoani walizalisha Asali Tani 2,135.9 zenye thamani ya Shs.2,178,570,000/= na Nta Tani 398.8 zenye thamani ya Shs.797,550,000/=. Changamoto tuliyonayo ni kuboresha taaluma ya ufugaji nyuki kwa kutumia mizinga na mbinu za kisasa. Elimu inatolewa kwa wafugaji nyuki kupitia programu za ugani ili waongeze viwango vya matumizi ya tekinolojia ya kisasa ya ufugaji nyuki kutoka asilimia 2 na kufikia walau asilimia 30 ifikapo Desemba 2010. Vyama vya Ushirika wa Wafuga Nyuki 25 vimeandikishwa. CHANGAMOTO ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA MIKAKATI YA KUDHIBITI UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA VYANZO VYA MAJI:
Mkoa umeainisha Changamoto za uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji na kuweka mikakati ya kudhibiti uharibifu usiendelee. (i) Uharibifu wa Mazingira Utokanao na Uvamizi wa Wafugaji na Wakulima Kwenye Hifadhi za Misitu na Vyanzo vya Maji . Zoezi la kuwaondoa wafugaji na wakulima waliovamia misitu ya hifadhi na vyanzo vya maji linaendelea kote Mkoani. Mifugo 80,144 sawa na 97% ya mifugo yote iliyokuwepo ndani ya hifadhi na vyanzo vya maji 133 imeondolewa. Aidha, Kaya 10,496 zenye watu 73,790 waliovamia Misitu ya Hifadhi zimeondolewa. Baadhi ya wavamizi katika Wilaya ya Urambo hawajaondolewa kwa sababu wameweka pingamizi Mahakamani kwa kile kinachodaiwa kuwa Vijiji vyao ambavyo vimo ndani ya Msitu wa Hifadhi wa Ulyankulu vimesajiliwa kisheria. Suala hili linashughulikiwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wilaya 4 (Uyui, Urambo, Sikonge na Nzega) zimeingizwa katika Mpango Shirikishi wa Usimamizi wa Misitu ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za misitu.
(ii) Uharibifu wa Mazingira Unaotokana na Ukataji Miti Kiholela kwa Ajili ya Kuni, Mkaa na Mbao: Maeneo yote ya uvunaji wa mazao ya misitu yametayarishiwa mpango wa uvunaji. Aidha, wananchi na Taasisi, hususan watumiaji wakubwa wa mkaa na kuni wamehamasishwa kuanzisha mashamba yao ya miti. Sanjari na hili, uhamasishaji wa kutumia majiko na mabani sanifu unaendelea kote Mkoani ukifanywa na Wataalamu wa Halmashauri kwa kusaidiana na AZAKI kama Total Land Care, Africare, CARITAS, World Vision nk.
(iii) Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Uhamishaji wa Mifugo Kiholela : Kila kijiji kimehimizwa kuwa na Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ambao utazingatiwa na wakazi wote. Kati ya Vijiji 488 ni Vijiji 26 tu ambavyo vimeshatayarisha mpango wa matumizi bora ya ardhi. Halmashauri za Wilaya zimehimizwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuzisaidia Serikali za Vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi. Aidha, wananchi wamehimizwa kutenga maeneo ya uoto wa asili kwa ajili ya malisho ya mifugo ( Ngitiri ). Hadi Juni 2009 jumla ya hekta 114,144 zimeshatengwa kwa ajili hiyo.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||