|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA MAJI:
9.1 Hali ya Huduma ya Maji: Juhudi za Serikali za katika kuboresha huduma ya Maji, zimekuwa zikiendelea katika maeneo mbalimbali hapa Mkoani Tabora ili kuhakikisha tunafikia lengo la MKUKUTA na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2003 katika kuongeza asilimia ya utatikanaji maji kufikia 65% kwa vijijini na 75% kwa mijini ifikapo mwaka 2009/2010. Juhudi hizo zinaendelezwa kupitia programu ya Maji na Usafi wa Mazingira kitaifa.
Hali ya Huduma ya Maji Vijijini. Hadi kufikia mwezi Desemba, 2009 asilimia 41 ya wakazi waishio vijijini wanapata maji safi na salama ikilinganishwa na asilimia 28.5 kwa mwaka 2005 ya wakazi wa vijijini ndio walikuwa wanapata huduma hii. Kiwango hiki ni chini ya lengo la MKUKUTA, la kufikisha huduma ya Maji vijijini kwa 65% ifikapo mwaka 2009/2010. Kutofikia kwa kiwango hicho kumetokana na ufinyu wa bajeti za maji, ugumu wa upatikanaji wa vyanzo vya maji vya kudumu na pia mwamko mdogo wa wananchi katika kutunza na kuendesha miradi ya maji mara inapokamilika na kukabidhiwa kwao na hivyo huicha ikiharibika. Hata hivyo kupitia fedha za mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji Serikali inaibua, kujenga na kukarabati miradi ya Maji ili kuhakikisha kunaongezeko la upatikanaji wa huduma ya Maji. Pia, tunazishauri halmashauri za Wilaya kutenga fedha za miradi ya maji kupitia bajeti zao za kila mwaka. Aidha, tunaendelea kutoa ushauri kwa Halmashauri za Wilaya na vijiji kuendeleza huduma ya maji kwa kuanzisha na kuendeleza mifuko ya maji ili iweze kumudu gharama za uendeshaji na matengenezo ya miradi yao. Hadi mwezi Desemba, 2009 vijiji 429 vilikuwa vimeanzisha mifuko ya maji kati ya vijiji 488 vyenye kamati za maji. Mifuko hiyo ilikuwa na jumla ya Shs. 95, 900,584.50 Katika kuendeleza upatikanaji wa huduma ya maji, Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishaji wa vyombo vya usimamizi na uendeshaji wa miradi (water user entities), ikiwa ni pamoja na Jumuiya za Watumiaji Maji na Kamati za Maji za Vijiji. Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji na kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira. Vilevile, wananchi wanashirikishwa katika kupanga na kutekeleza miradi yao ya maji.
Hali ya Huduma ya Maji Mijini: Kwa upande wa mijini hadi kufikia mwezi Desemba, 2009 asilimia 54 ya wakazi wake hupata huduma ya maji safi na salama ikilinganishwa na asilimia 36 kwa mwaka 2005. Kiwango hiki ni chini ya lengo la MKUKUTA, la kuongeza upatikanaji wa huduma ya Maji mijini kwa 75% ifikapo mwaka 2009/2010. Kutofikiwa kwa kiwango hicho kumetokana na ufinyu wa Bajeti za maji na uchache wa upatikanaji wa vyanzo vya maji vya kudumu. Kupitia mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji tayari mito yote katika Mkoa wa Tabora inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya Maji ili kuweza kupata vyanzo vipya ambavyo vitasaidia kuongeza ubora wa huduma ya maji katika miji.
Hali ya Mifumo ya Maji Taka: Mji wa Tabora ndio mji pekee wenye mfumo wa maji taka katika Mkoa, Mpaka sasa ni asilimia 6% ya wakazi wake wameunganishwa katika mfumo wa maji taka ikilinganishwa na 4.1% kwa 2003. Hata hivyo kiwango cha ongezeko bado ni kidogo ikilinganishwa na lengo MKUKUTA la kuongeza huduma hii kutoka 17% mwaka 2003 hadi 30% mwaka 2009/2010. Kutofikiwa kwa lengo hili kumetokona na wananchi kutokuelewa faida na umuhimu wa kuunganishwa katika mfumo huu, lakini pia suala la kiufundi nalo limechangia kwa kiasi kikubwa. Kupitia programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Mijini tayari kuna Mhandisi Mshauri aliyeajiriwa na mamlaka ya Maji safi na Maji taka mjini Tabora kufanya upembuzi ya yakinifu na kusanifu mradi huu ili kuhakikisha wananchi waishio mjini wanaunganishwa katika mfumo huu wa maji taka.
PROGRAMU NDOGO YA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI:Mkoa wa Tabora unatekeleza programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kuanzia mwezi Julai 2007. Katika kipindi cha Juni 2007 hadi Januari, 2010 Halmashauri za Wilaya zimepelekewa Tshs.4,725,883,814/= kutoka Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ili kugharimia utekelezaji wa miradi midogo midogo, kujenga uwezo na ukarabati na ujenzi wa ofisi za wahandisi wa maji. Sekretariat ya Mkoa pia imepelekewa Tshs.72,240,000/= katika kipindi cha Juni, 2007 hadi Januari 2010 fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kufanya ukaguzi, kutoa ushauri wa kiufundi na uratibu wa miradi inayotekelezwa.
9.3 Ujenzi wa Miradi ya Maji Vijijini:Katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2005 – 2010. Mkoa ulipanga kujenga na kukarabati miradi ya maji 174, ikiwa ni kujenga visima vifupi 81,kukarabati visima visima vifupi 23, Kujenga visima virefu 23, kukarabati mifumo ya maji ya bomba 17 , kujenga mifumo 25 ya uvunaji wa maji ya mvua na kujenga mifumo ya maji ya bomba 5. Hadi kufikia mwezi Desemba 2009, jumla ya miradi 760 ilikuwa imejengwa na kukarabatiwa kwa mchanganuo ufuatao; ikiwa ni visima vifupi 321,ukarabati visima vifupi 50, ujenzi wa visima virefu 215, ukarabati mifumo ya maji ya bomba 63, ujenzi wa mifumo 83 ya uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mifumo ya maji ya bomba 28. Mafanikio haya makubwa yametokana Mpango wa Maendeleo ya ya Sekta ya Maji wa mwaka 2006-2025 unaondelea kutekelezwa hapa Mkoani, lakini pia mwamko na mwitikio wa wananchi katika kushikiriki katika ujenzi na utunzaji wa miradi ya maji.
9.4 Fedha Zilizotumwa kwa Ajili ya Ujenzi wa Miradi ya Maji:Jumla ya Tshs.1,141,178,000/= zilitumwa katika mwaka wa fedha wa 2006/07 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika Halmashauri zote Mkoani Tabora. Jumla ya Tshs.1,442,268,780.00 zilitumwa katika kipindi cha mwaka 2008/09. Katika kipindi cha Mwezi Mei 2009 hadi Desemba 2009, Tshs.2,142,077,034.00 zimetumwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kulipia huduma zitakazotolewa na Wataalam washauri, ujenzi wa miradi, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi pamoja na uendeshaji wa ofisi.
9.5 Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Kitaifa:Programu hii inayogharamiwa na Serikali pamoja na wahisani mbalimbali, inatekelezwa katika Wilaya zote nchini. Kila Wilaya ilikwishachagua vijiji 10 ambapo miundombinu itajengwa. Mpaka sasa halmashauri zote sita za Mkoa zimekwisha ajili Wahandisi washauri (Consultants) tangu mwezi Novemba 2009 na tayari wahandisi washauri hao wanaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya maji katika maeneo husika, kazi hii ya awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2010. Baada ya hapo awamu ya pili ya ambayo ni ujenzi wa miuondombinu ya maji itaanza na itachukua takribani miaka miwili. Baada ya utekelezaji wa mardi katika vijiji 60 vya awali kukamilika vitachuguliwa tena vijiji 10 kutoka kila Wilaya. Wahandisi washauri walioajiliwa na Wilaya ni Howard Humphreys (Tanzania) Limited ambaye ameajiriwa na halmashauri za Wilaya za Igunga, Nzega,Tabora Manispaa, Sikonge na Urambo. NIMETA Consult (T) Limited ameajiliwa na halmshauri ya Wilaya ya Tabora Vijijini (Uyui).
9.6 Miradi Inayotekelezwa na Taasisi Nyingine:Jumla ya miradi 309 inayofadhiliwa na wadau mbalimbali (mashirika ya kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali) ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mingine imekamilika. Miradi hiyo ina thamani ya Tshs.1,329,435,595.75 bilioni na inatarajiwa kuhudumia watu wapatao 51,077 ujenzi utakapokamilika. Kati ya miradi hiyo 309 tayari miradi 95 imekamilika na inahudumia watu wapatao 23,750.
9.7 Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Mijini:
1. Tabora Manispaa: Mamlaka ya Majisafi na Majitaka mjini Tabora ndio wasimamizi wa utekelezaji wa programu hii katika Miji ya Tabora, Urambo na Sikonge. Mhandisi Mshauri (Consultant) Kampuni ya Balser & Hoffman kwa kushirikiana na Kampuni ya Wilalex wanaendelea kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na kupata gharama halisi za miradi katika miji ya Tabora, Urambo na Sikonge. Mtaalamu mshauri huyu pia amepewa kazi ya uboreshaji wa huduma ya maji katika mji wa Nzega hivi sasa kinachofanyika ni maandalizi ya mkataba mdogo kwa ajili ya kazi zitakazofanyika katika mji huo unaendelea na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Mhandisi mshauri amekwisha kamilisha upembuzi yakinifu na kusanifu miradi katika miji ya Sikonge, Urambo na Tabora mwezi Desemba, 2009. Kwa sasa mhandisi mshauri amewasilisha gharama halisi ya ujenzi wa miradi hiyo pamoja na michoro yake Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kupelekwa Benki ya Dunia kuombewa ‘No Objection' ili zabuni ya kumpata mkandarasi kwa ajili ujenzi wa miundombinu itangazwe.
Mji wa Igunga: Mji wa Igunga ulimpata Mtaalamu Mshauri mwaka 2004 na alikwisha fanya kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu na kupata gharama za kutekeleza mradi. Pia Mkandarasi wa kujenga miundombinu ya maji alikwishateuliwa na Halmashauri imekwisha saini naye Mkataba na ameanza kazi.
9.8 Mradi wa Maji unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo JICA : Katika kuhakikisha tatizo la huduma za Maji vijijini linapungua Mkoani Tabora, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia shirika lake la Maendeleo JICA wanafadhili mradi wa maji katika halmashauri zote sita katika Mkoa. Mradi huu umeanza kutekelezwa rasmi mwezi Septemba, 2009. Katika awamu ya kwanza ya mradi huu ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2011, kazi zitakazofanyika ni kuandaa Mpango wa Maji vijijini (Rural Water Plan) kwa Wilaya zote, kufanya upembuzi yakinifu na kusanifu wa Miradi ya Maji (hasa maji chini ya ardhi) katika Wilaya zote. Awamu ya ujenzi wa miundombinu ya Maji katika vijiji zaidi 65 ambavyo vitakuwa havina kabisa au vitaonekana vina matatizo makubwa ya Huduma ya Maji inatarajiwa kwanza mwezi Juni, 2011.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||