|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA MIFUGO:Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye mifugo mingi nchini ukiwa ni mkoa wa nne kwa wingi wa idadi ya mifugo ukifuatia mikoa ya Shinyanga, Mwanza, na Arusha. Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Taifa ya Kilimo (2002/2003), Mkoa wa Tabora ulikuwa na jumla ya Ng'ombe 1,454,717, Mbuzi 722,042, Kondoo 240,140, Kuku -1,962,306, Bata 83,536, Nguruwe 14,613, Punda 15,081, Mbwa 50,130 na Paka 19,856.
Shughuli za Maendeleo ya Mifugo Mkoani:Kwa kutambua mchango wa mifugo katika uchumi na maendeleo ya wafugaji, mkoa unaendelea kuratibu na kusimamia miradi mbali mbali ya sekta ya mifugo inayotekelezwa chini ya Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP) ikilenga kuinua kiwango cha ubora wa mifugo na hivyo kuongeza tija katika ufugaji. Aina ya miradi inayoibuliwa na kutekelezwa inajumuisha ujenzi wa Mabwawa na Majosho, kuinua Kosaafu za Mifugo ya asili, kuboresha malisho ya asili na kuzuia magonjwa ya mifugo.
UZALISHAJI WA MAZAO YA MIFUGO:Mazao ya mifugo ni Nyama, Ngozi, Maziwa, Mayai na Samli na kutokana na kosaafu za mifugo ya asili uzalishaji wa mazao mbali mbali ya mifugo ni wa kiwango cha chini. Hata hivyo, mauzo ya mazao ya mifugo yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2005/2006 mauzo yalikuwa Shs. 2,471,322,430/= na mwaka 2008/2009 mauzo yalifikia Shs. 9,598,010,650 /=. Aidha, elimu inaendelea kutolewa kwa jamii juu ya umuhimu wa kula mazao ya mifugo (nyama, maziwa na mayai) ambapo jumla ya wafugaji 944 wamepewa hamasa hii na kazi hii ya kuhamasisha jamii bado inaendelea katika Mkoa wote.
MASOKO NA BIASHARA NA MIFUGO:Biashara ya mifugo inafanyika katika Minada ya Msingi na ya Upili . Mwaka 2005/2006, Mkoa ulikuwa na jumla ya Minada 7 (Minada ya Msingi 5 na ya Upili 2). Kwa mwaka 2008/2009 Mkoa ulikuwa na jumla ya Minada 15 (Minada ya Msingi 13 na ya Upili 2). Kwa mwaka 2008/2009 wafugaji walipata pato la Shs.12,658,028,780/= kutokana na mauzo ya mifugo yao na Serikali ilikusanya mapato ya Shs.82,997,300/= kutokana na ushuru wa kusafirisha mifugo.
UENDELEZAJI WA VIZAZI (BREEDING):Shughuli za uendelezaji wa vizazi vya mifugo, hususan ng'ombe unafanyika kwa kiwango cha chini kwani kuna Madume Bora 88 ambayo ni machache yakilinganishwa na idadi kubwa ya majike ya asili yaliyoko Mkoani. Huduma za uhimilishaji hasa kwa ng`ombe zimeanzishwa na zinandelea kuhamasishwa na kutekelezwa kupitia katika Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo (DADPs) na vile vile kushirikisha sekta binafsi. Ili kuhakikisha kuwa njia hii inapewa msukumo wa peke yake, Viongozi wa Mkoa na Wilaya walifanya ziara ya mafunzo kwa kutembelea Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (National Artificial Insemination Centre) kilichoko Arusha ili kujifunza na hivyo kuongeza msukumo katika suala hili. Hata hivyo Kimkoa, kasi ya Uhimilishaji bado iko chini sana na jitihada zinaendelea kufanyika ili kupanua utekelezaji wa uzalishaji kwa njia ya Uhimilishaji ambapo Mkoa unalenga kuwa na Kituo cha Uhimilishaji katika kila kata na kwa kuanzia Mkoa ulilenga kuanza na jumla ya kata 25. Hadi sasa jumla ya kata 11 zinatoa huduma hii na juhudi za kuongeza idadi ya kata zenye kutoa huduma hii zinaendelea kuchukuliwa Kimkoa.
HALI YA MAGONJWA YA MIFUGO NA UDHIBITI WAKE:a) Nagana Mkoa wa Tabora una maambukizi ya kiwango cha juu cha ugonjwa wa Nagana unaoletwa na mbung'o. Hali hii inatokana na Mkoa kuwa na sehemu kubwa ni misitu ambayo haikaliwi na watu na hivyo kuwa makazi ya mbung'o. Jitihada zinachukuliwa kuua mbung'o katika maeneo yaliyo karibu na makazi ya watu kwa kuweka mitego inayowanasa na kuwaua. b) Magonjwa Yaletwayo na Kupe Magonjwa yaletwayo na kupe ni: • Ndigana kali (East Cost Fever), • Ndigana baridi (Anaplasmosis), • Kukojoa mkojo mwekundu (Babesiosis), • Moyo kujaa maji (Heart water), Magonjwa haya yanasababisha hasara kubwa kwa wafugaji kutokana na vifo vya mifugo na kuathiri ukuaji wake. Hali hii inatokana na udhaifu katika uogeshaji wa mifugo ambao ni wa chini kutokana na uchache wa majosho yanayotoa huduma Wafugaji wanahimizwa kuogesha mifugo yao mara kwa mara kwenye majosho ikiwa ni pamoja na kutumia pampu pale ambapo hakuna majosho. Pia matumizi ya dawa za kunyunyiza migongoni mwa mifugo ili kuzuia kupe yanahimizwa hasa pale pasipo na maji ya kutumia katika majosho. Ujenzi na ukarabati wa majosho unaendelezwa kupitia DADPs.
MIKAKATI YA KUDHIBITI MAGONJWA YA MIFUGO:(a) Kuwawezesha wafugaji kuibua miradi ya kufufua, kujenga na kuendesha majosho kwa kuunda vikundi imara vya wafugaji kwa ajili ya kumudu gharama za uendeshaji wa huduma za uogeshaji. Jumla ya majosho 53 yamekarabatiwa katika wilaya za Sikonge, Urambo, Uyui, Nzega, Igunga na Manispaa ya Tabora. Jumla ya majosho mapya 32 yamejengwa katika wilaya za Nzega, Urambo, Sikonge na Manispaa ya Tabora. Pia Mkoa unaendelea kutoa elimu kwa wafugaji ili wafuge kwa kufuata kanuni za ufugaji bora ambapo jumla ya vijiji 488 vya Mkoa huu vimepatiwa elimu hii kupitia huduma za ugani kwa kila wilaya. (b) Wafugaji wenye mifugo michache wanaelimishwa juu ya matumizii sahihi ya pampu za mgongoni katika kuzuia na kuua kupe sambamba na mafunzo juu ya matumizi ya dawa za kunyunyiza migongoni mwa mifugo zinazozuia kupe wasiwaume mifugo. (c) Kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 17 ya Magonjwa ya Mifugo ya Mwaka 2003 na Waraka wa Rais Na. 1 wa Mwaka 2002 unaoelekeza hatua za kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mifugo nchini. (d) Kusisitiza uogeshaji wa mifugo yote inayonunuliwa minadani kabla ya kusafirishwa kutoka eneo la mnada hasa katika minada iliyo karibu na majosho yanayofanya kazi.
MAGONJWA YA MIFUGO AMBAYO NI MAJANGA YA KITAIFA:i. Homa ya Mapafu ya Ng`ombe: Katika hatua ya kuutokomeza ugonjwa huu, Mkoa kupitia wilaya zake zote sita unachanja ng'ombe wote kwa kwa mtindo wa (ROLL BACK VACCINATION PLAN) kwa kutoa chanjo kwa kila mwaka.
ii. Mafua Makali ya Ndege (Highly Pathogenic Avian Influenza): Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege bado haujaonekana katika Mkoa wa Tabora lakini Mkoa uko katika moja ya njia kuu za Magharibi (western flyway) za ndege wahamaji kutoka Kaskazini mwa Bara la Afrika. Kwa kufahamu hali hii, Mkoa unachukua hatua za tahadhari kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inayoelekeza kutoa elimu kwa jamii juu ya viashiria hatarishi vya ugonjwa huu na tayari mabango na vipeperushi vyenye habari juu ya ugonjwa huu vimesambazwa Mkoani kote ikiwa ni pamoja na miongozo kwa walimu juu ya kuwafundisha wanafunzi wa shule za msingi kuhusu ugonjwa huu.
iii . Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever): Mkoa wa Tabora uko pembezoni mwa Bonde la Ufa. Hali hii inaufanya Mkoa huu kuwa katika uwezekano wa kupata maambukizi ya Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever). Hata hivyo mpaka sasa hakuna dalili za kuwepo kwa viashiria vya magonjwa ya Homa ya Bonde la Ufa. Hatua za tahadhari zinaendelea kuchukuliwa kwa kuwaelemisha wananchi na watu wote wanaoshughulika na uchinjaji/uchunaji wa wanyama. Kichaa cha Mbwa: Kichaa cha mbwa ni moja ya magonjwa hatari yanayoathiri watu na wanyama wa aina zote. Hatua zinazochukuliwa ili kudhibiti ugonjwa huu ni pamoja na kuchanja paka na mbwa mara moja kila mwaka sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu dalili ya ugonjwa huu na tahadhari zake.
(v). Ugonjwa wa Kideri (Sotoka ya Kuku): Ufugaji wa kuku unaathiriwa sana na ugonjwa wa Kideri (Sotoka ya kuku) kwa kusababisha vifo vingi vya kuku mara moja. Ili kukabiliana na ugonjwa huu, wafugaji wanaelimishwa kuchanja kuku, hususan kwa chanjo ya matone ya macho mara nne kwa mwaka na mwitikio wa wafugaji wa kuku ni mzuri.
HALI YA UPATIKANAJI WA MALISHO NA MAJI:Upungufu wa malisho ya asili na maji kwa matumizi ya mifugo hujitokeza zaidi katika kipindi cha kiangazi, Wilaya za Igunga na Nzega zinaathirika zaidi. Hali hii husababisha kuwepo kwa uhamishaji wa mifugo kwenda maeneo yenye malisho na kusababisha uvamizi wa maeneo ya Misitu ya Hifadhi. Ili kukabiliana na suala hili, elimu kwa wafugaji inaendelea kutolewa ili kila mmoja afuge kulingana na eneo lililopo. Aidha Mkoa unasisitiza kuinua ubora wa nyanda za malisho ya asili (Ngitile). Katika Mkoa kuna jumla ya hekta 94,848.5 za ngitile zilizotengwa na kuhifadhiwa na hutumika kwa malisho wakati wa kiangazi. Hata hivyo vijiji vinaendelea kuhimizwa kuwa na Mpango bora wa matumizi ya ardhi ambapo kila kijiji kinatakiwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji lakini mwitikio bado ni mdogo kutokana na ukweli kwamba utekelezaji wa Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999 na Na. 5 ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 bado hazijatekelezwa ipasavyo. Eneo lililokwisha tengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo Kimkoa katika wilaya za Nzega, Igunga, Urambo na Sikonge bado ni dogo sana linapolinganishwa na idadi kubwa ya mifugo kwani eneo hili huweza kulisha jumla ya ng'ombe 37,940 tu kati ya jumla ya ng'ombe 2,099,265 walioko katika Mkoa huu. Hii ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya mifugo katika maendeleo ya sekta Kimkoa. Msisitizo unawekwa ili ufugaji uende sawa sawa na uwezo wa eneo lililopo na siyo kuweka mifugo mingi kwenye eneo dogo.
HALI YA MWELEKEO WA UFUGAJI WA KISASA NA KIBIASHARAMkoa umeendelea kutumia fursa za ASDP na wadau wengine katika kutekeleza miradi mbalimbali ya ufugaji wa kisasa, hivyo kuwandaa wananchi katika ufugaji wa kibiashara. Juhudi inafanyika ya kuhamasisha wafugaji na wafanya biashara wa mifugo kuunda na kusajili vyama vya wafugaji na vyama vya wafanya biashara wa mifugo kwa lengo la kuhakikisha ufugaji unakuwa wa kisasa, endelevu na wa kibiashara na kupata masoko ya uhakika ya mifugo na mazao yake. Wafugaji wachache wamekuwa na mwamko wa kubadilisha ufugaji wao kwa kufuga ng`ombe na mbuzi wa maziwa na kuku wa mayai, pia kufuga Madume na Majogoo Bora kwa ajili ya kubadilisha koo za mifugo yao ya asili ili kuongeza uzalishaji. Ili kuelekeza ufugaji katika mwelekeo wa kibiashara na tija, Mkoa, kwa kutumia fedha za ASDP umeweza kutekeleza miradi mbali mbali ya kuendeleza mifugo. Wadau wengine wa wanaoshiriki katika uendelezaji wa mifugo ni Simmors, Africare, Tabora Development Fund Trust (TDFT), Heifer Project Tanzania na World Vision Tanzania.
PEMBEJEO ZA MIFUGO:(a) Maduka ya Dawa : Mkoa una jumla ya maduka 43 ya dawa za mifugo yakilinganishwa na jumla ya maduka 17 yaliyokuwepo mnamo mwaka 2005. Huduma hii inatolewa na sekta binafsi. Wafanyabiashara wa pembejeo za mifugo wanahamasishwa kufungua vituo vingi zaidi katika maeneo ya tarafa, kata na vijiji ili kusogeza huduma karibu na watumiaji wa huduma hizo. Aidha, Mkoa pia umekuwa ukipata dawa za ruzuku za kuogesha mifugo na kwa mwaka 2008/2009 Mkoa umepokea na kusambaza jumla ya lita 40,992 za dawa za aina mbali mbali za ruzuku kwa ajili ya kuogesha mifugo ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na kupe. (b) Vyakula vya Mifugo: Chakula cha ziada kwa ajili ya mifugo kinatokana na mashudu ya pamba na alizeti. Aidha kuna pumba za mahindi na mpunga zinazotumika katika kutengeneza chakula cha ziada kwa ng'ombe wa maziwa, mbuzi wa maziwa, kuku na nguruwe lakini wafugaji walio wengi bado hawajawa na mwamko wa kuwapatia mifugo yao chakula cha ziada.
IDADI YA MALAMBO:Katika kushughulikia tatizo la maji, uchimbaji na ukarabati wa malambo ni muhimu ili kuhifadhi maji kwa matumizi ya mifugo. Kupitia Mpango wa DADPs na PADEP wananchi wanaendelea kuibua miradi ya uchimbaji malambo. Mkoa una malambo 196 na mabwawa 48. Hali hii inaonyesha uhaba wa miundombinu hii ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya mifugo. Ili kukabiliana na hali hii, Mkoa unahimiza Wilaya zote kuwa na mipango shirikishi jamii ya kufufua malambo na mabwawa chakavu yanayoweza kufanyiwa ukarabati na pia kuangalia uwezekano wa kuchimba mabwawa mapya kupitia fedha za ASDP na ufadhili wa wadau wengine wa Sekta ya Mifugo na wakati huo huo kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya mifugo. Jumla ya mabwawa 17 yamekarabatiwa, mabwawa 30 yamejengwa na mabirika ya kunyweshea mifugo yamejengwa katika wilaya za Igunga, Urambo, Manispaa ya Tabora na Sikonge. Mafanikio haya yanatokana na matumizi ya fedha za DADPs kwa kujenga miundo mbinu ya skimu za umwagiliaji ambapo kunawekwa sehemu ya kunyweshea mifugo.
UZALISHAJI WA MIFUGO:Zaidi ya asilimia 95 ya mifugo yote inayofugwa Mkoani ni mifugo ya asili iliyo na sifa mbali mbali zinazoifanya jamii ya wafugaji kupendelea kuwafuga wanyama hawa licha ya uzalishaji mdogo. Wanyama hawa kwa silika yao hawana mwelekeo wa kumfanya mfugaji kuondokana na tatizo la umaskini kutokana na uzalishaji wa kiwango cha chini unaosababishwa na ukoosafu wao. Ili kubadilisha mifugo, Mkoa unahimiza uboreshaji wa mifugo kwa njia ya kuinua koosafu za mifugo ya asili. Suala la kuinua ukoosafu wa mifugo linatiliwa mkazo mkubwa ili kuwa na mifugo chotara wenye ukoosafu bora zaidi kwa kutumia madume, majogoo na mabeberu bora; pia msukumo zaidi unawekwa katika matumizi ya uzalishaji wa ng'ombe kwa njia ya Uhimilishaji.
CHANGAMOTO ZA SEKTA YA MIFUGO MKOANI:Mifugo katika Mkoa wa Tabora bado haina tija kwa wafugaji. Changamoto kuu zinazochangia uzalishaji usio na tija ni pamoja na hizi zifuatazo: (i) Upungufu wa eneo la nyanda za malisho na miundo mbinu ya kuvuna maji ya mvua kulingana na idadi ya mifugo iliyopo. Magonjwa ya mifugo hususan yale yanayosababishwa na viini vya magonjwa yanavyoenezwa na kupe. Huduma za ugani kutowafikia wafugaji kwa kiwango kikubwa. Ukoosafu duni wa mifugo ya asili. Ukosefu wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya mifugo. Ukosefu wa wawekezaji katika machinjio ya Manispaa ya Tabora. Machinjio hii ilijengwa katika miaka ya 1980 lakini ujenzi wake haukukamilishwa. Vyombo vya fedha kutokuwa tayari kuwakopesha wafugaji wadogo wadogo.
MIKAKATI YA KUENDELEZA MIFUGO MKOANI:1. Kuweka bayana majukumu ya kila mdau. 2. Kubaini na kutangaza maeneo tengefu yanayofaa kwa shughuli za uwekezaji katika mkoa ili kuvutia wawekezaji kuwekeza katika ufugaji wa ranchi ndogo ndogo 3. Kuhamasisha wananchi waunde vikundi vya wasindikaji wa mazao mbali mbali ya mifugo hususan maziwa na ngozi ili kupanua wigo wa soko la bidhaa hizo kwa kuyaongezea thamani baada ya kusindikwa. 4. Kila wilaya kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo maeneo maalumu kwa ajili ya ufugaji yatabainishwa na kuendelezwa kuwa nyanda bora za malisho zitakazofugiwa wanyama kwa kuzingatia uwezo wa nyanda za malisho sambamba na idadi ya mifugo inayotakiwa (Rangeland Carrying capacity). 5. Kuboresha Miundombinu yote muhimu kwa ajili ya maendeleo ya mifugo itawekwa katika hali nzuri kwa ajili ya matumizi. Miundombinu itakayozingatiwa kwanza ni Majosho, Malambo ya kuvuna maji ya mvua, Mabirika ya kunyweshea mifugo na Vibanio vya kudumu kwa ajili ya shughuli za kitaalamu katika kudhibiti magonjwa ya mifugo kwa njia ya chanjo. 6. Kufufua na kujenga vituo vipya vya maendeleo ya Mifugo ngazi ya Kata(Ward Livestock Development Centres -WLDCs). 7. Kuanzishwa nafasi ya Afisa Maendeleo ya Mifugo ngazi ya Tarafa (Divisional Livestock Development Officer) ambaye kazi yake itakuwa ni kuratibu shughuli za maendeleo ya mifugo katika Tarafa yote akiziunganisha Kata zote katika tarafa hiyo. 8. Kuweka mtandao wa mawasiliano katika ngazi zote za utendaji ndani ya Halmashauri za wilaya mtandao ambao utatumainika wakati wote. 9. Kuhamasisha jamii katika ngazi zote ili jamii ijenge tabia ya kula mazao ya mifugo hususan kunywa maziwa, kula mayai na nyama kwa wingi. 10. Kuimarisha huduma za ugani wa Mifugo zinazotumainika na endelevu 11. Kuanzisha, kuimarisha na kusimamia Mashamba Darasa ya Mifugo. katika Wilaya zote za Mkoa wa Tabora kuanzia msimu ujao wa fedha. 12. Kuimarisha uzalishaji wa mifugo bora kwa njia ya Uhamilishaji. 13. Kuimarisha Viwanda na Masoko ya Mifugo katika Mkoa wa Tabora kwa kubaini na kutangaza fursa zilizopo zinazoweza kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kwa ajili ya kufungua viwanda vya kusindika mazao ya mifugo kama vile Maziwa, Nyama na Ngozi, Pembe na hata Kwato. 14. Kuendeleza ufunguzi wa Minada mingi ya awali (primary livestock markets).
MAENDELEO YA UVUVI WA SAMAKI:Mkoa wa Tabora hauna vyanzo vikubwa kwa ajili ya uvunaji wa viumbe wa majini hususan samaki. Katika Mkoa kuna jumla ya mito 11 na mabwawa 10 ambamo shughuli za uvuvi zinafanyika na jumla ya wavuvi 1,627 ndio wanaofanya shughuli za uvuvi katika vyanzo hivyo. Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi katika Mkoa wa Tabora yanakwamishwa na kutokuwa na vyanzo vya kudumu vya maji kwani kiasi kikubwa cha mito na mabwawa hukauka wakati wa kiangazi na kusababisha kusimama kwa shughuli za uvuvi. Kwa upande wa mabwawa, kuna jumla ya mabwawa (10) ambayo ni Igombe na Kazima katika Wilaya ya Tabora, Mibono, Uluwa, Igigwa na Utyatya katika Wilaya ya Sikonge, Sagara Wilaya ya Urambo, Loya katika Wilaya ya Uyui na Mwanzugi na mbuga ya Wembere katika Wilaya ya Igunga. Shughuli za uvuvi hufanywa na wavuvi binafsi kwa sehemu kubwa na kwa kiasi kidogo shughuli hizo zinafanywa na vikundi vinane (8) ambavyo wavuvi hawa wamejinga kwa lengo la kuunda SACCOS na hivyo kuwa katika hali nzuri ya kupata mikopo na kujiendeleza zaidi. Aidha, ili kuongeza vyanzo vya samaki Mkoa umechukua jukumu la kuhamasha jamii juu ya kuwa na ufugaji wa samaki katika maeneo yao wenyewe kwa kuchimba malambo ya kufugia samaki. Hadi sasa Mkoa una jumla ya wafugaji 130 walio na jumla ya mabwawa 247 ya kufugia samaki. Ili kuhakikisha kuwa wafugaji hawa wanapata mbegu bora za samaki, Mkoa umekwisha ainisha eneo maalumu litakalojengwa lambo kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki vyenye ubora na hatimaye kuwagawia wafugaji binafsi na taasisi mbali mbali zinazojishughulisha na ufugaji wa samaki. Eneo limekwisha patikana huko Igombe na kinachofuata sasa ni kuishirikisha Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ili kujenga muundo mbinu huo na sgughuli ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki uanze mara baada ya kukamilisha ujenzi wa lambo hilo. Katika kuhakikisha kuwa hakuna matumizi ya zana haramu za uvuvi zinazotumika katika kuvua samaki kwenye mito na mabwawa yaliyoko Mkoani, Mkoa umekwishatoa waraka kwa kila wilaya kuhakikisha kuwa wauzaji wote wa zana za uvuvi katika kila wilaya wanaagizwa kutouza zana zisizokubalika katika kuvua samaki na kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka hayo na kwenye maeneo ya uvuvi ili kuhakikisha kuwa hakuna muuzaji au mvuvi anayeuza au kutumia zana haramu katika kuvua. Vile vile, Mkoa umeunda kikosi maalumu cha Doria kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika maduka na kwenye maeneo ya uvuvi kwa lengo la kudhibiti matumizi ya zana haramu za uvuvi katika Mkoa. Kikosi cha doria cha Mkoa kinaundwa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kikosi cha kuzuia ujangiri wa wanayama pori na askari polisi. Aina ya samaki wanaopatikana katika vyanzo vichache vilivyopo Mkoani ni samaki aina za Kambale, Sato, Perege na Kamongo na kwa wastani mavuno ya samaki aina zote kwa mwaka ni tani 874.2
Changamoto zinazoikabili Sekta ya Uvuvi. Changamoto zilizopo ni ugumu katika kuitikia uhamasishaji wa uundaji na uimarishaji wa Vyama Vya Wavuvi ambavyo vitaunda SACCOS ili viweze kupata mikopo kwa ajili ya kujiendeleza vema katika shughuli za uvuvi. Hadi Desemba 2009, Mkoa umewezesha kuundwa kwa vikundi 8 vya wavuvi vinavyohamasishwa ili kuunda SACCOS. Matumizi ya zana haramu za uvuvi. Mkoa umeweza kutoa elimu ya matumizi ya zana bora za uvuvi kwa wakulima 1,268 ili waepuke matumizi ya zana haramu za uvuvi. Aidha ni mahitaji ya Mkoa kuwa ufugaji wa samaki na viumbe maji wengine unatiliwa mkazo na kuendelezwa na hivyo sekta ya uvuvi kupewa msukumo mkubwa katika jitihada za kuongeza vyanzo vya maji kwa njia ya ufugaji jamii na pia kupandikiza aina nyigine ya samaki katika vyanzo vilivyopo baada ya kuwa tumefanya mawasiliano na vituo vya utafiti wa samaki ili kujua ni aina zipi za samaki zinafaa kupandikizwa wapi na lini katika Mkoa wa Tabora.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||