|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA KILIMO:
Mkoa huzalisha mazao ya chakula na biashara ambayo ustawi wake hutegemea mvua.
Mazao ya Chakula : Mazao makuu ya chakula yanayolimwa ni Mahindi, Mpunga, Mtama, Muhogo, Viazi vitamu na Maharagwe.
Mazao ya Biashara : Mazao makuu ya biashara yanayolimwa ni Tumbaku, Pamba, Karanga, Alizeti na Vitunguu. Ziada ya mazao ya chakula hususan Mpunga, Mahindi na Maharagwe huuzwa kibiashara.
UZALISHAJI WA MAZAO: Kilimo katika Mkoa wa Tabora kwa kiasi kikubwa hutegemea mvua. Mvua zinazonyesha mara nyingi si za kutabirika kwa maana ya kiasi chake na mtawanyiko wake.Katika msimu wa 2008/2009, mvua zimeendelea kunyesha kutokea Novemba hadi Mei 2009. Mtawanyiko huo umewezesha kilimo cha mpunga hasa katika majaruba ya asili ambayo hujaa maji ya mvua kwa ajili ya kuustawisha hadi kuiva.
MALENGO YA KILIMO MSIMU WA 2008/2009: Katika msimu wa kilimo wa 2008/2009 Mkoa ulijiwekea lengo la kulima na kutunza hekta 521,451 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kuvuna tani 961,967. Lengo hilo la uzalishaji wa mazao ya chakula lilijumuisha tani 602,871 za nafaka, tani 348,658 za mazao ya mizizi na tani 32,436 za mazao ya mikunde. Ilitarajiwa kuwa malengo haya ya uzalishaji yakifikiwa Mkoa utaweza kujitosheleza kwa chakula katika msimu wa 2009/2010 kwa asilimia 130. Aidha, Mkoa ulijiwekea lengo la kulima hekta 176,398 za mazao ya biashara zilizotarajiwa kuvuna tani 187,761 .
UTEKELEZAJI WA MALENGO YA KILIMO MSIMU WA 2008/2009: Utekelezaji wa malengo ya kilimo, msimu wa 2008/2009 utajulikana baada ya tathmini ya utekelezaji wa malengo na uzalishaji wa mazao kufanyika, kuanzia mwezi Mei 2009. Baada ya tathmini Mkoa utakuwa umepata taarifa ya hali halisi ya utekelezaji wa malengo na vilevile ya uzalishaji wa mazao ya chakula na mazao ya biashara.
MATUMIZI YA ZANA NA PEMBEJEO, MWAKA 2008/2009 (a) Zana Sehemu kubwa ya wakulima Mkoani Tabora wanatumia jembe la mkono kama zana kuu ya kulimia. Matumizi ya zana za wanyamakazi yanaendelea kuhimizwa; kuna majembe 63,772 na makwama 15,865 ya kukokotwa na wanyamakazi. Kuna jumla ya matrekta makubwa na 180 matrekta madogo 15. Matrekta yaliyopo Mkoani yanatumiwa zaidi kusafirisha mizigo kuliko kulima. Mkoa unaweka msukumo ili matrekta yaliyopo yatumike kikamilifu ili kuongeza eneo linalolimwa na matrekta kwa mwaka. Sekta binafsi, hususan wauzaji wa matrekta madogo, wanashirikishwa katika kuhamasisha matumizi ya matrekta hayo kwa kufanya maonyesho ya matumizi ya matrekta hayo. Matumizi ya zana za kukokotwa na wanyamakazi yanaendelea kuongezwa kupitia Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo. Vile vile Taasisi binafsi zinashiriki kikamilifu katika upanuzi wa matumizi ya wanyamakazi katika kilimo. Kampuni ya 'Aliance One' nayo inawakopesha wakulima jozi moja ya maksai pamoja na zana. Mikopo hii inatolewa bila riba.
b) Pembejeo: Wastani wa Matumizi ya pembejeo, hususan mbegu bora na mbolea bado ni chini. Matumizi ya mbegu bora ni asilimia 19 ya mahitaji ya mbegu. Kwa upande wa mbolea za viwandani, matumizi ni asilimia 45 ya mahitaji. Matumizi ya samadi ni tani 396,911. Pembejeo zenye Ruzuku Musimu wa 2008/2009: Katika msimu wa 2008/2009 wakulima wa Tumbaku waliendelea kupata mbolea yenye ruzuku aina NPK kwa ajili Kilimo cha Tumbaku. Kwa upande wa mazao ya chakula, Wilaya ya Sikonge pekee ndiyo ilikuwa katika mpango wa kupatiwa pembejeo za ruzuku kwa ajili ya kilimo cha mahindi. Jumla ya wakulima 10,000 walikuwa katika mpango wa kupatiwa pembejeo za ruzuku kwa utaratibu wa kila mkulima kupatiwa: Kilo 10 za mbegu bora Mbolea ya kupandia (DAP au Minjingu) Mbolea ya kukuzia (UREA)
HALI YA CHAKULA MSIMU 2008/2009: Mahitaji ya chakula Mkoani katika msimu wa 2008/2009 yalikuwa tani 531,681. Chakula kilichozalishwa msimu 2007/2008 kilikuwa tani 600,380 ambazo zimetosheleza mahitaji ya wakazi wa Mkoa na ziada ya tani 70,689. Hata hivyo kuna Vijiji katika Tarafa ya Mwakalundi, Wilayani Nzega, Vijiji katika Tarafa ya Tabora Kusini, Wilayani Tabora na Vijiji katika Tarafa ya Uyui, Wilayani Uyui vilizalisha pungufu kulinganisha na mahitaji yao. Wilaya zilichukua hatua za kuhakikisha usalama wa chakula na kukabiliana na upungufu katika ngazi ya kaya kwa kufanya yafuatayo: - kutoa elimu ya ukadiriaji wa mahitaji ya chakula kwa mwaka katika ngazi ya kaya sambamba na uhifadhi bora wa chakula - kuwaelimisha wananchi kuhusu uwezekano wa bei za chakula kupanda kutokana na upungufu wa chakula duniani. - kuelimisha wananchi kuepukana na uuzaji holela na matumizi yasiyo ya lazima kwa mazao ya chakula. - kufuatilia wafanyabiashara kwa mazao ya chakula ili kuzuia wafanyabiashara toka nje ya nchi.
HALI YA CHAKULA MSIMU 2009/2010: Hali ya chakula Mkoani katika msimu wa 2009/2010 itafahamika baada ya tathmini ya mazao shambani kufanyika na kukamilika. Tathmini hiyo imepangwa kufanyika kuanzia mwezi Mei,2009. La sivyo kuna dalili njema ya Mkoa kupata mavuno mazuri ya chakula.
UNUNUZI WA MAZAO MAKUU YA BIASHARA: Mazao makuu ya biashara Mkoani Tabora ni Tumbaku, Pamba, Karanga na Alizeti. Mazao ya Tumbaku na Pamba yananunuliwa kwa mifumo inayosimamiwa na Bodi za mazao hayo. Mazao ya Karanga na Alizeti yananunuliwa kwa mfumo huria ambao una ugumu wa kufuatilia takwimu za mauzo. Kilimo cha Tumbaku kinapungua kutokana na wakulima wa zao hilo kushindwa kukidhi makubaliano ya kilimo cha Mkataba. Kilimo cha Mkataba kinamtaka mkulima kuuza mazao yake kwa kampuni iliyomkopesha pembejeo. Baadhi ya wakulima hukiuka utaratibu huu na hivyo kupoteza sifa ya kukopesheka. Ununuzi wa Tumbaku umeendelea kupanda na kushuka kutokana na hali ya hewa na idadi ya wakulima, wakati ununuzi wa pamba umeendelea kupanda kutokana na kuimarika kwa bei.
Miradi ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo: Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo: Mkoa wa Tabora unatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP) ambapo Halmashauri 6 za Mkoa wa Tabora zimepokea fedha kutoka ASDP kutekeleza Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo (DADPs).
Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola (Mbola Millenium Village Project): Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola uko katika Wilaya ya Uyui. Mradi huu unatekelezwa katika eneo la Vijiji 15. Mradi unatoa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo cha Mahindi, ambazo ni mbegu bora, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia. Mafanikio makubwa ya uzalishaji kwa eneo yamepatikana, uzalishaji kwa eneo umeongezeka toka magunia 2 – 5 kwa ekari na kufikia magunia 25 – 30 kwa ekari. Zaidi ya Kaya 6,000 zimefaidika kutokana na mradi huu.
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA ASDP: Baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa kutokana na utekelezaji wa ASDP katika Mkoa wa Tabora ni pamoja na: Kuboresha huduma za ugani kwa wakulima kutokana na upatikanaji wa vyombo vya usafiri, pikipiki 15 na baiskeli 17 na utumiaji wa mbinu ya mashamba darasa ambapo kila Wilaya inaendesha mashamba darasa kati ya 20 hadi 40 kwa musimu. Kupanda kwa tija katika mashamba ya wakulima walioshiriki katika mashamba darasa; kwa zao la mahindi uzalishaji uliongezeka toka magunia 2 – 5 kwa ekari na kufikia magunia 15 – 20 kwa ekari. Kuongezeka miundombinu mbalimbali ya sekta ya kilimo kama vile maghala 11, soko 1, majosho 2 na malambo 24. Kupatikana mashine na zana mbalimbali kama vile matrekta 5, zana jozi 23 za kukokotwa na wanyamakazi na mashine 7 za kukamua mafuta ya alizeti. Kuongeza kilimo cha umwagiliaji ambapo miradi midogo 70 ya kilimo cha bustani imeimarishwa. Kupungua kwa matukio ya magonjwa ya mifugo kutokana na kuongezeka huduma za chanjo na uogeshaji. Uboreshaji wa mifugo ya asili umeanza hususan kuku na ng'ombe; majogoo bora 860 na madume bora 67 ya ng'ombe yamepatikana . Pia huduma ya uhamilishaji imeanzishwa. Kuna uelekeo wa mafanikio makubwa zaidi kupatikana kutokana na ASDP. Mkoa umedhamiria kushughulikia changamoto kuu za kilimo kwa awamu, badala ya kuweka shabaha nyingi kwa wakati mmoja.
MPANGO WA KUENDELEZA KILIMO MWAKA 2008/2009: Katika msimu wa 2008/2009 Halmashauri za Mkoa wa Tabora zilipangiwa kupata jumla ya Shs.2,621,378,004/= toka ASDP kwa ajili ya k utekeleza Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo (DADPs). Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya wanyamakazi katika vikundi 36, kujenga malambo 8, kujenga/kukarabati majosho 15, kuendesha mashamba darasa 126, kuzalisha mbegu bora katika vikundi 27, ununuzi wa pikipiki 37 na ujenzi wa vihenge bora 18. Fedha za ASDP zilizopokelewa hadi kufikia Septemba 2008 ni Shs.775,460,490/=. Pia, Mkoa kupitia Halmashauri zake, umetenga fedha kwa ajili ya kununulia matrekta makubwa 6 na matrekta madogo 35, yote pamoja yana thamani ya Shs.452,870,000/=. Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo hapa chini:
Kilimo cha Umwagiliaji:Mkoa wa Tabora hauna mito ya kudumu, kwa hali hiyo umwagiliaji unafanywa kwa kukinga maji ya mvua. Umwagiliaji unaofanyika sio umwagiliaji kamili, bali ni uvunaji wa maji toka kwenye mikondo ya asili inayopitisha maji wakati wa mvua. Kilimo hiki ni cha majaruba, hususan kwa zao la mpunga katika mabonde, ambayo yanapatikana katika Wilaya zote za Mkoa wa Tabora. Mkoa una jumla ya skimu 18 za umwagiliaji zenye jumla ya ukubwa wa karibu hekta 5,000 ambapo zao kuu linalolimwa ni mpunga. Mbinu zinazotumika kupata maji kwa ajili ya umwagiliaji ni mabwawa, mabanio katika mito, malambo na visima. Umwagiliaji wa matone umeanza kutumika Mkoani kwa kiwango kidogo katika Wilaya ya Urambo.
Mikakati ya Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji: Njia muafaka ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Tabora ni ujenzi wa mabwawa. Halmashauri zinaendelea kufanya utafiti wa awali na upembuzi yakinifu wa maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Tabora. Baada ya usanifu wa miradi kukamilika, maandiko ya miradi yanawasilishwa TAMISEMI/Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ajili ya kuombewa fedha toka Ruzuku ya Umwagiliaji ya Wilaya (DIDF) na Ruzuku ya Umwagiliaji ya Taifa (NIDF). Katika msimu wa 2008/2009 jumla ya miradi 7 imeombewa fedha.
2.12 Utafiti wa Kilimo:UTAFITI WA KILIMO: Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tumbi kiko Mkoani Tabora katika Wilaya ya Tabora. Wakulima wananufaika moja kwa moja na matokeo ya tafiti shirikishi (on-farm research) zinazofanywa na kituo hiki katika Wilaya zote Mkoani. Kituo hiki kinaendelea na tafiti mbalimbali kwa kushirikisha wakulima. Tafiti hizo ni pamoja na: Kilimo misitu Majaribio ya aina 4 za mbegu za mahindi ambazo ni TMV1, SITUKA1, SITUKA M1 na KILIMA. Kutafuta mbegu za mahindi zenye ukinzani dhidi ya magugu aina ya kiduha. Halmashauri za Mkoa wa Tabora zimehimizwa kuwashirikisha watafiti katika michakato ya uandaaji wa mipango ya Wilaya ya kuendeleza kilimo. Vilevile Kituo cha Utafiti cha Tumbi kinahimizwa kuboresha mbinu za utoaji wa matokeo ya tafiti zao kwa wakulima.
CHANGAMOTO ZA SEKTA YA KILIMO MLOANI: Sekta ya Kilimo Mkoani Tabora inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na: Idadi ndogo ya Maafisa Ugani isiyokidhi mahitaji. Hadi Juni 2008 Mkoa ulikuwa na Maafisa Ugani wa fani ya kilimo wapatao 145. Watumishi waliopo katika ngazi ya Kata ni 98 tu wakati huo huo kuna jumla ya Vijiji 488 na Kata 135. Ili kuwa na angalau mtaalamu mmoja wa fani ya kilimo katika kila Kata, kuna upungufu wa wataalamu 37. Vijana wengi wanaoishi Vijijini wanashughulika na biashara ndogondogo badala ya kushiriki katika kilimo na wengine wanahamia mijini na hivyo kupunguza nguvukazi Vijijini. Wakulima hutumia pembejeo kwa kiwango kidogo hususan mbegu bora na mbolea kutokana na uwezo mdogo wa kumudu bei za pembejeo hizo. Kupungua kwa idadi ya wakulima wa Tumbaku kutokana na kushindwa kuzingatia masharti ya kilimo cha Mkataba. Fursa zilizopo kama vile ASDP zinatumiwa kwa mtazamo wa kusambaza rasilimali kidogo kidogo ili kugusa maeneo mengi kwa wakati mmoja. Hali hii haiwezeshi kuona matokeo ya fursa kwa urahisi. Wakulima kutumia jembe la mkono kama zana kuu ya kulimia. Hali hii inawafanya wakulima kutumia nguvu nyingi na kwa ufanisi mdogo katika kilimo.
MIKAKATI YA KUENDELEZA KILIMO MKOANI: Mkoa ulipanga na ukaendesha Kongamano la Kilimo lililoshirikisha wadau wa Kilimo ili kupata mbinu muafaka za kufanikisha yafuatayo: Kuimarisha mbinu shirikishi za utoaji ugani ili kuwafikia wakulima katika vikundi, na pia kuwawezesha wakulima kuwa wakulima wakufunzi. Kuimarisha usimamizi wa kilimo kwa kuhusisha ngazi zote za uongozi na za kiutawala. Kuhamasisha wakulima kujiunga katika ushirika wenye nguvu ili waweze kupata huduma katika taasisi za fedha. Juhudi za kuanzisha Benki ya Ushirika Mkoani Tabora zinaendelea ambapo kamati ya maandalizi imeundwa. Kuhamasisha uzalishaji wa mbegu bora za Daraja la Kuazimiwa (Quality Declared Seeds) katika ngazi ya kaya. Kuwaandaa wakulima kuelekeza nguvu katika matumizi ya zana za wanyama kazi na hatimaye matrekta. Kuelekeza raslimali katika maeneo haya machache yenye matokeo yaliyo dhahiri katika kuleta mapinduzi katika kilimo.
|
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||