|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA KILIMO:
Maafisa Ugani wa Kilimo : Mkoa wa Tabora unao jumla ya wataalam 133 wa fani mbali mbali za kilimo. Idadi hii ni ndogo kwa kuzingatia kwamba Mkoa una Kata 135 na sasa Vijiji 524. Mgawanyo wa wataalam wa kilimo ni kama ifuatavyo: Ofisi ya Mkoa – 1, Makao Makuu za Halmashauri – 47, ngazi ya Kata – 60 na ngazi ya Vijiji – 25. Halmashauri zinaendelea na juhudi za kuboresha usafiri wa Maafisa Ugani kuwawezesha kuwafikia na kuwahudumia zaidi wakulima wengi. Hadi kufikia Juni, 2010 Maafisa Ugani wa Kilimo 51 wanatumia usafiri wa pikipiki. Juhudi za kuwaendeleza maafisa ugani kitaaluma zinafanyika. Katika kipindi cha kuanzia 2005/2006 hadi 2009/2010 jumla ya maafisa ugani 35 wamesomeshwa mafunzo ya muda mrefu katika viwango vya stashahada, shahada na shahada ya uzamili.
Huduma za Ugani: Mbinu kuu inayotumika kutoa huduma za ugani ni Mashamba Darasa. Jumla ya mashamba darasa 716 yameendeshwa katika kipindi cha kuanzia msimu wa 2005/2006 hadi 2009/2010. Mkoa unaimarisha vituo vya kufundishia wakulima ambapo kuna Vituo vya Wanyamakazi 6 na Vituo vya Kata vya Rasilimali za Kilimo 15. Mkakati wa Kusimamia Kilimo Mkoani Tabora: Mkoa umejipanga kuongeza msukumo katika kilimo kwa kuweka Mkakati wa Kusimamia Kilimo. Mkakati unawataka Viongozi na Watendaji katika ngazi zote kuwa na ratiba za kusimamia kilimo. Takwimu muhimu za kilimo zitakusanywa na kutunzwa katika Madaftari ya Kilimo ngazi za Kitongoji, Kijiji, Kata na Halmashauri. Pia kumbukumbu za utendaji kazi wa Afisa Ugani zitatunzwa katika Daftari la Afisa Ugani. Malengo ya Mkakati wa Kusimamia Kilimo Mkoani Tabora ni: Kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ugani kwa wananchi vijijini. Kuongeza matumizi ya zana bora na pembejeo za kilimo. Kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na ushirika wa wakulima katika kilimo. Kuwapo na mpango wa matumizi bora ya ardhi. Kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kupanua kilimo cha umwagiliaji.
Mazao ya Chakula : Mazao Makuu ya Chakula yanayolimwa ni Mahindi, Mpunga, Mtama, Muhogo, Viazi Vitamu na Maharagwe.
Mazao ya Biashara : Mazao Makuu ya Biashara yanayolimwa ni Tumbaku, Pamba, Karanga, Alizeti na Vitunguu. Ziada ya mazao ya chakula hususan Mpunga, Mahindi na Maharagwe huuzwa kibiashara.
UZALISHAJI WA MAZAOKilimo katika Mkoa wa Tabora kwa kiasi kikubwa hutegemea mvua. Mvua zinazonyesha mara nyingi si za kutabirika kwa maana ya kiasi chake na mtawanyiko wake. Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji kwa eneo (tija) kwa mazao makuu ya chakula ambayo ni mahindi na mpunga. Kwa wastani, tija katika zao la mahindi imeongezeka kutoka tani 0.9 kwa hekta mwaka 2005/2006 hadi tani 1.5 kwa hekta mwaka 2008/2009; ambapo tija katika zao la mpunga inaongezeka kutoka tani 3 kwa hekta mwaka 2005/2006 hadi tani 5.5 kwa hekta mwaka 2008/2009. Katika msimu wa 2009/2010 mvua zilianza kunyesha mwezi Novemba. Mvua zimeendelea kunyesha kwa kiwango cha wastani hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Januari. Palitokea kusimama kwa mvua kati ya Januari mwishoni na mwanzoni mwa Februari, 2010 ambapo mazao yameathirika katika baadhi ya maeneo. Wilaya zinafanya tathmini ya athari za kiangazi hicho. Mkoa unatarajia kupata chakula cha kutosha endapo mvua zinazonyesha hivi sasa zitaendelea mpaka mwezi Machi. Mwaka jana (Msimu wa 2008/2009), Mkoa ulikuwa na ziada ya Tani 70,689 za Chakula baada ya mavuno. Aidha, palitokea mlipuko wa viwavi jeshi mwanzoni mwa mwezi Januari katika sehemu za Wilaya za Nzega, Urambo, Sikonge, Uyui na Tabora. Wadudu hao walidhibitiwa mapema na hivyo hawakusababisha athari kubwa katika uzalishaji wa mazao.
MALENGO YA KILIMOKatika msimu wa kilimo wa 2009/2010 Mkoa ulijiwekea lengo la kulima na kutunza hekta 558,688 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kutoa mavuno ya tani 1,042,749 . Lengo hilo la uzalishaji wa mazao ya chakula linajumuisha tani 635,896 za nafaka, tani 369,857 za mazao ya mizizi na tani 36,996 za mazao ya mikunde. Hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Desemba 2009, jumla ya hekta 328,574 za mazao ya chakula zimelimwa, sawa na asilimia 59 ya malengo. Utekelezaji huo unatarajiwa kuongezeka kwa vile kilimo cha mpunga, mhogo na viazi vitamu bado kinaendelea. Aidha, Mkoa umejiwekea lengo la kulima hekta 192,768 za mazao ya biashara zilizotarajiwa kutoa mavuno tani 214,001 . Utekelezaji wa malengo ya kilimo cha mazao ya biashara hadi kufikia Machi, 2010 ni hekta 132,366 sawa na 69%. Utekelezaji unatarajiwa kuongezeka kwa sababu kilimo cha Alizeti na Dengu bado kinaendelea.
Matumizi ya Zana na Pembejeo:(a) Zana Sehemu kubwa ya wakulima Mkoani Tabora wanatumia jembe la mkono kama zana kuu ya kulimia. Matumizi ya zana bora za kilimo yanaendelea kuhimizwa na yanaongezeka. Mkoa umeweka msukumo kuongeza idadi ya matrekta na kuhimiza matrekta yaliyopo yatumike kikamilifu. Idadi ya matrekta makubwa yanayofanya kazi imeongezeka toka 144 mwaka 2005/2006 na kufikia Matrekta 275 mwaka 2009/2010. Katika kipindi hicho idadi ya matrekta madogo (power tillers) imeongezeka toka 7 mwaka 2005/2006 hadi 97 mwaka 2009/2010. Mkoa unahimiza matumizi ya wanyamakazi katika shughuli za kilimo. Zana za wanyamakazi zilizopo ni pamoja na majembe 64,315 ya plau na mikokoteni 1,107. b) Pembejeo: Matumizi ya pembejeo, hususan mbegu bora na mbolea bado yako chini. Mkoa unaendelea kuhimiza matumizi ya pembejeo ili kuongeza tija katika kilimo. Matumizi ya mbolea za viwandani yameongezeka toka tani 13,477 msimu wa 2005/2006 na kufikia tani 19,414 msimu wa 2008/2009 ongezeko la 44%. Matumizi ya mbegu bora pia yameongezeka katika kipindi hicho toka tani 976 hadi tani 1,549 ongezeko la 50%. Matumizi ya mbegu bora na mbolea katika msimu wa 2009/2010 hadi kufikia Januari, 2010 yamefikia tani 1,876 za mbegu mbalimbali na tani 23,079 za mbolea za viwandani. Pia matumizi ya samadi yamefikia tani 854,657. Mahitaji ya Mkoa kwa mwaka 2009/2010 ni tani 3,854 za mbegu bora na tani 44,763 za mbolea za viwandani. Kumekuwa na changamoto ya upungufu wa mbolea hususan kwa kilimo cha tumbaku. Hali hii imetokana na idadi ya wakulima wa tumbaku kuongezeka kulinganisha na idadi iliyotumika wakati wa kufanya makisio ya mahitaji ya pembejeo. Idadi ya wakulima waliojisajili kulima tumbaku imeongezeka toka 24,677 msimu wa 2008/2009 hadi 35,273 msimu wa 2009/2010.
c) Pembejeo zenye Ruzuku : Mkoa umeendelea kupata Pembejeo za Ruzuku kupitia Utaratibu wa Vocha katika msimu wa 2009/2010. Mazao yaliyolengwa katika utaratibu wa ruzuku ni Mahindi, Mpunga na Pamba. Ruzuku kwa ajili ya zao la Mahindi imetolewa katika Wilaya za Sikonge na Urambo, ruzuku ya Mpunga imetolewa katika Wilaya ya Igunga na ruzuku ya Pamba imetolewa katika Wilaya za Igunga, Nzega, Urambo na Uyui. Ruzuku iliyotolewa inatosha uzalishaji katika ekari 35,300 za mahindi; ekari 3,000 za mpunga na ekari 100,940 za pamba. Kupatikana kwa pembejeo za ruzuku kumeamsha ari ya matumizi ya mbegu bora na mbolea. Kuna muitikio mkubwa katika utumiaji wa vocha za ruzuku. Pia sekta binafsi imejitokeza kikamilifu kusambaza pembejeo za ruzuku.
HALI YA CHAKULAHali ya chakula Mkoani kwa msimu wa 2009/2010 ni nzuri kutokana na mavuno ya msimu wa 2008/2009. Mkoa ulivuna jumla ya tani 553,160 za mazao ya chakula katika msimu wa 2008/2009; uzalishaji huo ulikuwa ni 111% ya mahitaji ya chakula kwa mwaka 2009/2010. Hata hivyo kulikuwa na maeneo yaliyozalisha chakula chini ya mahitaji yao kwa mwaka. Mkoa hautarajii kuwa na upungufu wa chakula katika kipindi kilichobakia cha 2009/2010 kwa vile mahindi yameanza kukomaa katika baadhi ya maeneo wakati maharagwe, karanga na viazi vitamu vimeanza kuvunwa. Wilaya zinachukua hatua za kuhakikisha usalama wa chakula na kukabiliana na upungufu katika ngazi ya kaya kwa kufanya yafuatayo: Kutoa elimu ya ukadiriaji wa mahitaji ya chakula kwa mwaka katika ngazi ya kaya sambamba na uhifadhi bora wa chakula. Kuna jumla ya maghala 139 Vijijini na kaya 41,739 zinazotumia Vihenge bora. Kuelimisha wananchi kuepukana na uuzaji holela na matumizi yasiyo ya lazima kwa mazao ya chakula. Kuhamasisha kilimo cha kiangazi, hususan mazao ya bustani. Katika kipindi cha 2005/2006 hadi 2009/2010 jumla ya vikundi 127 vimewezeshwa kuboresha kilimo cha bustani. Kufanya ufuatiliaji wa karibu katika maeneo yaliyoathiriwa na hali mbaya ya hewa. Kamati za maafa katika ngazi mbalimbali zinahusika katika ufuatiliaji wa hali ya chakula katika maeneo yao.
UNUNUZI WA MAZAO MAKUU YA BIASHARA:Mazao makuu ya biashara Mkoani Tabora ni Tumbaku, Pamba, Karanga na Alizeti. Mazao ya Tumbaku na Pamba yananunuliwa kwa mifumo inayosimamiwa na Bodi za mazao hayo. Mazao ya Karanga na Alizeti yananunuliwa kwa mfumo huria ambao una ugumu wa kufuatilia takwimu za mauzo. Wakulima waliojisajili kulima Tumbaku kwa msimu wa 2009/2010 wameongezeka kutoka kaya 24,677 msimu wa 2008/2009 na kufikia kaya 35,273. Sababu za ongezeko hilo ni: Wakulima wamevutiwa na bei ya tumbaku katika msimu wa 2008/2009. Wakulima wamevutiwa na utaratibu wa kupata pembejeo kupitia benki badala ya utaratibu wa zamani ambapo makampuni ya ununuzi ndiyo yalikuwa yakikopesha pembejeo. Vyama 7 vya Msingi vilivyokuwa vimesinzia vimefufuliwa.
MIRADI YA KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO: Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo: Mkoa wa Tabora unatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) ambapo Halmashauri 6 za Mkoa wa Tabora zinapokea fedha kutoka ASDP kutekeleza Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo (DADPs). Katika msimu wa 2009/2010 Mkoa ulitarajia kupokea jumla ya shilingi 3,534,060,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo. Mchanganuo wa fedha hizo ni: Ruzuku ya Uwekezaji – 1,386,708,000/=, Ruzuku ya Kujenga Uwezo – 771,666,000/=, Ruzuku ya Huduma za Ugani – 334,374,000/= na Mfuko wa Umwagiliaji – 1,041,312,000/=. Miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2009/2010 ni pamoja na kujenga miradi 4 ya umwagiliaji, majosho 4, malambo 10, masoko 3 na maghala 2; kudhibiti magonjwa ya mifugo, kuendesha mashamba darasa 87, kununua pikipiki 20, kununua trekta kubwa 1 na mtrekta madogo 39, na kuendesha huduma za uhamilishaji katika wilaya zote 6. Vile vile uendelezaji wa ujenzi wa skimu 4 za umwagiliaji utafanyika.
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA ASDP: Baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa kutokana na utekelezaji wa ASDP katika Mkoa wa Tabora tangu 2006/2007 ni pamoja na: Kuboresha huduma za ugani kwa wakulima kutokana na upatikanaji wa vyombo vya usafiri; Magari 2, Pikipiki 33 na Baiskeli 70 na utumiaji wa mbinu ya Mashamba Darasa 149 katika utoaji wa huduma za ugani. Kupanda kwa tija katika mashamba ya wakulima walioshiriki katika mashamba darasa; kwa zao la Mahindi uzalishaji umeongezeka toka magunia 2 – 5 kwa ekari na kufikia magunia 15 – 20 kwa ekari. Kuongezeka kwa miundombinu mbalimbali ya sekta ya kilimo kama vile Maghala 13, Masoko 5, Majosho 20, Malambo 25, Kliniki za Mifugo 2, Mtambo 1 wa Biogas na ujenzi wa Vituo vya Kata vya Rasilimali za Kilimo 5. Kupatikana kwa mashine na zana mbalimbali kama vile Matrekta makubwa 2 na Matrekta madogo 66, jozi 51 za Maksai na zana za kukokotwa na wanyamakazi na Mashine 13 za kukamua mafuta ya alizeti. Kuongezeka kwa Kilimo cha Umwagiliaji kutoka hekta 3,748 mwaka 2005/2006 hadi hekta 8,040 mwaka 2009/2010 ongezeko la 115%. Jumla ya miradi midogo 70 ya Kilimo cha Bustani imeimarishwa, miradi mikubwa 4 imekarabatiwa, miradi 4 mipya inajengwa, miradi 8 imefanyiwa upembuzi yakinifu na vikundi 9 vinatumia Umwagiliaji wa Matone. Kuanzishwa kwa Huduma ya Uhamilishaji katika Wilaya zote 6. Kuanzishwa kwa Uzalishaji wa Mbegu Bora za Muhogo, Viazi Vitamu Mtama na Alizeti; pia ukuzaji wa vitalu vya miche bora ya miembe na michungwa.
Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola (Mbola Millenium Village Project): Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola unatekelezwa kuanzia Septemba, 2006 ndani ya vijiji 15 vilivyomo katika Kata nne za Tarafa ya Ilolangulu, Wilaya ya Uyui. Eneo la vijiji vya Mbola lina ukubwa wa kilometa za mraba 1,334 zenye kaya 6,000 na wakazi wapatao 34,000. Azma ya mradi huu ni kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ili kuboresha hali ya maisha ya jamii na kupunguza umaskini ifikapo mwaka 2015. Mradi huu unatekelezwa kwa mbinu shirikishi jamii na unachangiwa na Washirika wa Maendeleo kupitia shirika la United Nations Human Security Trust Fund (UNHSTF), Millennium Promise (MP) na Chuo Kikuu cha Columbia chini ya uratibu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Washirika wa Maendeleo huchangia asilimia 55 ya gharama zote, na Serikali inachangia asilimia 18, mashirika yasiyoya kiserikali asilimia 18 na wanakijiji wanachangia asilimia 9. Kwa hesabu ya uwekezaji wa mradi wa milenia, mtu mmoja hugharamiwa $110 kwa mwaka, ambazo huchangiwa na wadau mbali mbali (Washirika wa Maendeleo $50, Serikali $30, NGOs $20, Jamii $10).
Mafanikio ya Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola: Mradi umeweza kutoa mafunzo na huduma za ugani katika kila kaya ili kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula hasa mahindi na mazao ya biashara kama Karanga, Alizeti, Pamba, Viazi Vitamu na Muhogo. Katika misimu ya 2006/07 na 2007/08, kila kaya iliwezeshwa ruzuku ya pembejeo za kilimo ( kilo 10 za mbegu bora ya mahindi, kilo 50 za mbolea ya kupandia na kilo 100 za mbolea ya kukuzia) Katika msimu wa 2007/08, mradi ulitoa jumla ya kilo 10,000 za mbegu ya pamba kwa wakulima 1,000 kila mkulima kilo 10, pia mbolea ya kupandia aina ya DAP kilo 50 kwa kila mkulima aliyelima zao la pamba. Kuongezeka uzalishaji wa Mahindi toka chini ya tani moja kwa hekta kabla ya mradi kuanza hadi wastani wa tani 3.4 kwa hekta kwa mwaka wa kwanza wa mradi, na kufikia wastani wa tani 5.9 kwa hekta mwaka wa Pili wa mradi. Kila mkulima aliyepewa pembejeo za kilimo alichangia magunia 2 ya mahindi kuwa chakula cha wanafunzi shuleni. Kwa mwaka 2007/08 maguni 9,746 yalikusanywa. Wakulima na Viongozi wa Vijiji wamepata mafunzo kuhusu kilimo bora cha bustani, uvunaji wa mazao na utunzaji bora ili kupunguza upoteaji wa nafaka gharani. Zaidi ya miche 200,000 ya miti mbalimbali ikiwemo miti ya matunda, miti ya kurutubisha ardhi na kuni imepandwa katika maeneo ya Shule, Zahanati, Kituo cha Afya na pia kwa wakulima binafsi. Majogoo bora 765 yalisambazwa kwa Wafugaji wa Kuku wa asili. Kuku wameongezeka katika eneo la mradi kutokana na jamii kuchanja kuku wote kuepuka ugonjwa wa kideri (New Castle) kila baada ya miezi mitatu hadi minne. Jumla ya Wafugaji Nyuki 316 wenye uwezo wa kuzalisha lita 61,225 kwa mwaka wametambuliwa na mikakati ya kuwaendeleza inafanyika. Wafugaji Nyuki 32 wamepatiwa mafunzo ya Ufugaji Bora wa Nyuki na vifaa vya kisasa. Kikundi cha Maendeleo Endelevu Mbola (MEMBO) kimekopeshwa mashine mbali mbali (trekta la kukokotwa kwa mikono, mashine za kukoboa na kusaga mahindi, Mashine za kukamua mafuta ya alizeti na jenereta ya umeme). Chama cha Kuweka na Kukopa, Mbola Millennium SACCOS, kimeanzishwa na mchakato wa kuanzisha benki ya vijiji umeanza. Vikundi mbali mbali vimewezeshwa kufanya biashara kama kuuza taa zinazo tumia Mwanga wa Jua (solar lanterns) kwa ajili ya kutoa mwanga na kuchaji simu za kiganjani. Kuweka mipango mkakati ya kujasirisha shughuli nyingi zilizopo katika eneo la mradi, ikiwemo uanzishwaji wa pembejeo kwa njia ya mkopo (input credit system) ilianza msimu wa kilimo wa mwaka 2008/09.
Kilimo cha Umwagiliaji:Mkoa wa Tabora hauna mito ya kudumu, kwa hali hiyo umwagiliaji unafanywa kwa kukinga maji ya mvua. Mkoa una jumla ya Skimu za Umwagiliaji 23 zenye jumla ya ukubwa wa hekta 8,040. Zao kuu linalolimwa katika skimu za umwagiliaji ni Mpunga. Mbinu zinazotumika kupata maji kwa ajili ya umwagiliaji ni Mabwawa, Mabanio katika mito, Malambo na Visima. Umwagiliaji wa Matone umeanza kutumika Mkoani ambapo jumla ya ekari 9 zinamwagiliwa na mavuno yanapatikana mara 3 katika msimu mmoja wa kilimo.
Mikakati ya Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji: Njia muafaka ya kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji katika Mkoa wa Tabora ni ujenzi wa mabwawa. Halmashauri zinaendelea kufanya utafiti wa awali na upembuzi yakinifu wa maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Tabora. Katika msimu wa 2009/2010 skimu 4 zinajengwa na 2 zinakarabatiwa. Kukamilika kwa skimu hizo kutaongeza hekta 1,400 zinazomwagiliwa. Wilaya zinaendelea kutafuta uwezekano wa kuboresha skimu za umwagiliaji zinazotumia mabanio katika mito ya msimu kupata mabwawa ili kuongeza uhakika wa uzalishaji.
UTAFITI WA KILIMO:Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tumbi kiko Mkoani Tabora katika Wilaya ya Tabora. Wakulima wananufaika moja kwa moja na matokeo ya tafiti shirikishi (on-farm research) zinazofanywa na kituo hiki katika Wilaya zote Mkoani. Kituo hiki kinaendelea na tafiti mbalimbali kwa kushirikisha wakulima. Tafiti hizo ni pamoja na: Kilimo misitu. Majaribio ya mbegu za Mahindi, Alizeti, Muhogo, Karanga na Viazi Vitamu. Kutafuta mbegu za mahindi zenye ukinzani dhidi ya magugu aina ya kiduha.
Halmashauri za Mkoa wa Tabora zimehimizwa kuwashirikisha watafiti katika michakato ya uandaaji wa Mipango ya Wilaya ya Kuendeleza Kilimo ili kuibua miradi ya utafiti. Vilevile Kituo cha Utafiti cha Tumbi kinahimizwa kuboresha mbinu za utoaji wa matokeo ya tafiti zao kwa wakulima, ikiwa ni pamoja na kushirikisha Wilaya katika vikao vya ushauri. CHANGAMOTO ZA SEKTA YA KILIMO:Sekta ya Kilimo Mkoani Tabora inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na: Kilimo cha kutegemea mvua ambapo uzalishaji huathiriwa na hali ya hewa isiyotabirika. Wataalam wachache waliopo kutotumika kikamilifu. Tija ndogo katika kilimo kutokana na matumizi madogo ya mbolea na mbegu bora. Kutofuatwa kwa kalenda ya kilimo kunakotokana na matumizi ya zana duni (jembe la mkono) katika kilimo.
MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA KILIMO KWANZA:Mkoa umeandaa Mfumo wa Utekelezaji wa Nguzo 10 za KILIMO KWANZA. Mikakati ya utekelezaji imewekwa kwa kuzingatia Majukumu yote yaliyobainishwa katika KILIMO KWANZA. Mkoa umejipanga kusukuma utekelezaji wa KILIMO KWANZA kwa kjiwekea Mkakati wa Kusimamia Kilimo. Mkakati wa Mkoa unatekelezwa kuanzia msimu wa 2009/2010. Mkoa umeanza utekelezaji wa Nguzo 10 za KILIMO KWANZA na pia kufanya maandalizi mbalimbali ya kuhakikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA.
Utekelezaji wa Nguzo 10 za KILIMO KWANZA: Mkoa umetekeleza yafuatayo kwa kuzingatia Nguzo za KILIMO KWANZA: Mfumo wa Utekelezaji wa Nguzo 10 za KILIMO KWANZA umeandaliwa katika ngazi za Mkoa na Wilaya. Mkoa umejiwekea Mkakati wa Kusimamia Kilimo. Mkakati unatekelezwa kuanzia msimu wa 2009/2010 kwa kuhusisha Viongozi na Wataalam katika ngazi zote. Mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika ya Mkoani unaendelea kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata huduma za kibenki kwa masharti nafuu. Wilaya zimebainisha mazao ya kipaumbele yatakayopewa msukumo ili kuongeza tija katika kilimo. Pembejeo zenye ruzuku zimetolewa na Serikali za kutosha uzalishaji wa ekari 35,300 za Mahindi, ekari 3,000 za Mpunga na ekari 100,940 za pamba kwa msimu wa 2009/2010. Wilaya zimeunda Timu za kufuatilia shughuli za kilimo kuanzia msimu wa 2009/2010. Vituo 15 vya Kata vya Rasilimali za Kilimo vimeanzishwa na vinaimarishwa ili kutumika kujenga mitandao ya wadau wa kilimo na kutolea mafunzo kwa wakulima. Mfumo wa utoaji wa maarifa za utekelezaji wa KILIMO KWANZA umewekwa. Taarifa hizo zitawasilishwa katika vikao vya Kamati za Ushauri za Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa.
Maandalizi yafuatayo yanafanyika ili kuhakikisha utekelezaji wa KILIMO KWANZA:
Bajeti za Halmashauri za mwaka 2010/2011 zitazingatia utekelezaji wa KILIMO KWANZA. Mkoa unaendeleza juhudi za kuongeza uhakika wa uzalishaji katika kilimo kwa kuongeza kilimo cha umwagiliaji. Maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yanafanyiwa upembuzi yakinifu ili kutafuta fedha kwa ajili ya kuyaendeleza. Ili kuinua uwezo wa kiuchumi kwa wakulima wadogo, wakulima wanahamasishwa kujiunga katika ushirika ili kuwa na nguvu ya pamoja. Halmashauri zimehimizwa kutenga bajeti kwa ajili ya uimarishaji wa ushirika. Wilaya zimehimizwa kutenga fedha kwa ajili ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi mijini na vijijini. Mipango hiyo itahakikisha uhifadhi wa mazingira katika uendelezaji wa kilimo na pia kutoa fursa ya kupatikana kwa ardhi kwa ajili ya Uwekezaji wa Kilimo. Kushirikiana na SIDO katika kuongeza thamani ya mazao kwa kutumia teknolojia mbalimbali za usindikaji. Kushirikiana na taasisi za kifedha zinazotoa fursa ya kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||