|
||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII:
Mkoa umekuwa ukiratibu shughuli mbalimbali za Maendeleo ya Jamii ikiwa ni pamoja na mikopo ya Wanawake na Vijana, uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo, kuratibu shughuli za Ukimwi, kuratibu shughuli za Asasi, Ujenzi wa Nyumba Bora, maswala ya Jinsia na watoto. MIKOPO KWA AKINA MAMA NA VIJANA:Mwaka 2006 – hadi Desemba 2009 wanawake na vijana wamepata mikopo ya jumla ya Tshs.295,485,418/=. Fedha ambayo imekwisha rejeshwa ni Tshs.171,000,265/= sawa na 58%, bado kurejeshwa Tshs.124,485,153/= arobaini na mbili (42%). Hii ikiwa ni pamoja na riba ya asilimia 10. Aidha hadi kufikia, Desemba 2009 jumla ya vikundi vya wajasiriamali 185 vimeanzishwa, SACCOS 14 na VICOBA vimeanzishwa.
Ujenzi wa Nyumba Bora:Kuanzia mwaka 2005 Desemba 2009, jumla ya nyumba bora 6460 zimejengwa. Aidha kupitia vikosi vya ujenzi wananchi wanaendelea kuhamasishwa kujenga nyumba kwa kutumia tofari za kuchoma, moramu iliyochanganywa na simenti kidogo na kutumia pumba kama nishati mbadala kuepuka matumizi ya kuni. Asasi Zisizo za Serikali (AZISE):
Katika Mkoa wa Tabora Asasi zisizo za Kiserikali zimekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla Mafanikio: Wanawake wameweza kuwapatia watoto wao wanaosoma mahitaji muhimu ya shule. Kujenga nyumba bora za familia, hivyo kubadili sura ya Mkoa kwa kuwa na nyumba bora.. Kupunguza makali na ugumu wa maisha ndani ya familia. Kuweka akiba Benki. Kutokana na mikopo, wanawake wameweza kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ya sikukuu za Kitaifa mfano Sabasaba na Maonyesho ya SIDO. Wananchi walio wengi wamefahamu umuhimu wa ujenzi wa nyumba bora. Wananchi wamepata ajira kwa Mfano: Asasi ya Health Action Promotion Organization (HAPO), JIDA, Tabora NGO's Cluster, AFRICARE na Bulding Resources Across Communities (BRAC) Kwa kupitia Asasi watoto yatima na waishio katika mazingira magumu wamepata mahitaji ya shule na wengine kupelekwa shule kwa mfano: HAPO inasomesha watoto 40 na Friends of Urambo and Mwanhala (FUM) watoto zaidi ya 90. Asasi kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) wanaendelea kufanya jitihada za kutokomeza ajira mbaya kwa watoto. Baadhi ya Asasi hizo ni TDFT na CARE FOR THE CHILD Wilayani Urambo. Hadi kufikia mwezi Desemba 2009 jumla ya watoto 4,700 wametolewa katika ajira mbaya. Aidha watoto waliokuwa na umri wa kwenda shuleni wamepelekwa shule.
CHANGAMOTO: Mwitikio mdogo wa watu kutokana na mitaji midogo na umaskini wa kipato. Vikundi vingi vimeshindwa kurejesha mikopo kwa wakati. Utumiaji mikopo kinyume na malengo. Usafiri husababisha ugumu wa kufuatilia mikopo kwa maeneo yaliyo mbali na Wilaya. Bajeti finyu inayosababisha baadhi ya vikundi kutokupata mkopo. Asasi nyingi hazina mitaji na kutegemea wafadhili kwa asilimia kubwa hivyo kushindwa kumudu kazi zao. Kuibuka kwa Asasi zinazokiuka taratibu, kanuni na sheria za uendeshaji.
MIKAKATI YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO: Mkoa unahamasisha Mashirika mengine yajitokeze kutoa mikopo yenye riba nafuu. Aidha yaliyopo yaendelee kutoa mikopo kwa riba nafuu kwa mfano; PRIDE, FINCA, SAMIDE, CARTAS, SIDO na BRAC Tanzania. Mkoa unafuatilia mara kwa mara kwa vikundi vilivyochukua mikopo. Elimu kwa wakopaji inaendelea kutolewa juu ya urejeshaji wa mikopo na elimu juu ya faida zitokanazo na mikopo. Elimu inatolewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa ujenzi wa Nyumba Bora. Wananchi wanahamasishwa kutumia pumba kuchoma tofari badala ya kuni ili kulinda mazingira. Halmashauri zinaendelea kuimarisha vikosi vya ujenzi vilivyopo na kuunda vikosi hadi Ngazi ya Kata. Halmashauri zinasimamia na kufuatilia shughuli zinazofanywa na Asasi. Halmashauri zinahakikisha Asasi zinatoa taarifa sahihi za shughuli zao kila Robo mwaka. Mkoa wa Tabora utambuzi wa Watoto Waishio katika Mazingira Hatarishi uliokwishafanyika ni jumla ya Watoto 42,495 walitambuliwa, kati ya hao wanaopata Huduma ni 39,061 ambazo ni sare za shule, kulipiwa ada za shule, mafunzo ya ufundi, kulipiwa kadi ya Afya ya Jamii (CHF) na chakula. Huduma zote zinafanywa na kuratibiwa na Halmashauri za Wilaya na Manispaa kwa kushirikiana na Asasi zisizo za Kiserikali (AZISE) zilizopo Mkoani Tabora.
MASUALA MTAMBUKA:UKIMWI: Tangu Serikali ilipotangaza UKIMWI kuwa ni Janga la Kitaifa Mkoa wa Tabora unaendelea kufanya jitihada ya kupambana na janga hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Mashirika mbalimbali na Asasi za Kiraia ndani na nje ya Mkoa zinajitoa kwa hali na mali kupambana na janga hili. Baadhi ya wadau hao ni TACAIDS kupitia RFA, UNDP, BENJAMIN WILLIAM MKAPA HIV/AIDS FOUNDATION, EGPAF na MILDMAY INTERNATIONAL. Shughuli zinazoendelea kufanyika ni pamoja na elimu kwa jamii juu ya njia za maambukizi na jinsi ya kujikinga, hamasa juu ya upimaji wa hiari baada ya kupata ushauri nasaha, huduma ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa UKIMWI (ARVs). Mkoa pia unahamasisha shughuli za UKIMWI mahali pa kazi.
JANUARI - DESEMBA, 2009 Jumla ya watu 95,448 walijitokeza kupima kwa hiari: Wanaume - 25,715 Wanawake - 38,344
Watu waliogundulika na VVU/UKIMWI: Jumla ya watu 4,314 waligundulika kuwa na VVU: Wanaume - 1,611 Wanawake - 2,703 Ushamiri [prevalence] wa VVU kwa watu waliojitokeza kupima ni 6.6 Waliokuwa wakipata huduma ya ARVs 1,820 sawa na asilimia 23.1. Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hizi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikiana na Taasisi ya Benjamini William Mkapa HIV/Aids Foundation inatekeleza Mradi wa ajira ya dharura unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) katika kupambana na Kifua Kikuu, Ukimwi na Malaria Mkoani Tabora.
MAFANIKIO KATIKA MASUALA YANAYOHUSU UKIMWI: Huduma za chakula na dawa zimetolewa kwa wananchi waishio na VVU/UKIMWI. Vikundi vya watu waishio na VVU/UKIMWI vimeundwa. Watoto Yatima wameweza kupata mahitaji muhimu ya shule mf. Ada, Sare na vifaa vya Shule. Hali ya Maambukizi imeshuka kutoka asilimia 9 kwa Mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 6.4 kwa utafiti wa mwaka 2007/2008. Hii ni kutokana na juhudi za Serikali na wadau mbalimbali kuwapatia wananchi elimu, hamasa juu ya upimaji wa hiari, huduma ya ARVs na lishe kwa wenye VVU, huduma kwa mama wajawazito (PMTCT) na huduma za nyumbani kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Home Based Care). Kuongezeka kwa vituo vya kupima VCT na PMTCT
CHANGAMOTO: Mpaka sasa Ugonjwa wa Ukimwi hauna dawa Ugonjwa wa Ukimwi unasababisha ongezeko kwa idadi ya watoto yatima na waishio katika mazingira magumu. Kukosekana kwa fedha ya kuwasaidia waishio na VVU/UKIMWI kuwa na mitaji ya kuanzisha shughuli za kudumu. Mwamko mdogo wa wafanyakazi kupima kwa hiari na kujua afya zao. Maambukizi bado yako juu kwa upande wa Wanawake
MIKAKATI:• Kuwa na Kampeni ya kudumu ya vita dhidi ya Ukimwi na ufuatiliaji wa Huduma kwa watu waishio na VVU/UKIMWI kuanzia ngazi ya Kitongoji. • Kuendelea kutoa hamasa zaidi kwa watumishi wajitokeze kupima Afya zao. • Ukimwi kuwa agenda ya kudumu katika vikao, mikutano yote kuanzia Ngazi ya Kitongoji. • Kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kuwapatia mitaji na huduma muhimu watu waishio na VVU/UKIMWI ili waweze kuendesha shughuli za kudumu. Elimu ya UKIMWI kutolewa hadi ngazi ya vijiji na vitongoji kupitia gari ya Sinema.
MPANGO WA SERIKALI WA KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI:Mikopo iliyotolewa SACCOS kupitia CRDB – Tshs.483,600,000/= ya awamu ya kwanza ilinufaisha wananchi 310. Mikopo kwa SACCOS 7 kupitia SCCULT – tshs.250,000,000/= kwa awamu ya pili. Kuna Tshs.100m/= zipo kwa ajili ya SACCOS za Wilaya ya Urambo SCCULT inaandaa utaratibu wa kuwakopesha wananchi. Mikopo ya fedha za Benki ya CRDB kwa SACCOS Tshs.3,871,258,000/=. Mikopo kwa wananchi fedha za Serikali (Mabillioni ya JK) iliyotolewa kupitia Benki ya NMB ni Tshs.283,165,000/=. Jumla ya wananchi 260 walikopeshwa fedha hizo. Urejeshaji wa mikopo siyo wa kuridhisha katika Wilaya ya Nzega na Tabora. Viongozi wa matawi hayo ya benki wanafuatilia urejeshwaji wa fedha hizo.
UWEZESHAJI WA WAJASIRIAMALI:Katika kipindi cha Mwaka 2005 – 2009, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Tabora limewawezesha Wajasiriamali kwa kuwapa mafunzo mbalimbali, vitendea kazi viwandani, mikopo, kuandaa na kuwezesha ushiriki wa Maonyesho ya bidhaa mbalimbali yaliyoandaliwa Kitaifa na Kimataifa. Katika kipindi hicho huduma mbalimbali zilitolewa kwa washiriki 915 Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limetoa jumla ya mikopo 1,034 ikiwa na thamani ya Tshs. 541,640,000/= ambayo imetoa jumla ya ajira 1,844 Uendelezaji wa Teknolojia (Artisans Support Program):Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 jumla ya vikundi 60 vya mafundi wadogo (Artisans) katika Wilaya zote 6 za Mkoa wa Tabora viliwezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi vya msaada na SIDO kupitia ushirikiano uliopo kati ya SIDO na Shirika lisilo la Kiserikali la Uingereza liitwalo Tools For Self Reliance (TFSR). Vifaa hivyo (Working Tools) vilitolewa kwa Wajasiriamali wanaojihusisha na ufundi na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama vile Wahunzi, Seremala, Ufumaji, Fundi Cherehani, Uchomeaji Vyuma, Utengenezaji wa Baiskeli na Ushonaji wa Bidhaa za Ngozi.
MAONYESHO YA BIASHARA:Katika kipindi cha Mwaka 2005 – 2009, jumla ya Wajasiriamali 245 kutoka Mkoa wa Tabora walihamasishwa na kushiriki Maonyesho mbalimbali yaliyoandaliwa ndani na nje ya nchi
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||