|
||||||||||||||||||||||
|
||||||||||||||||||||||||||||||
SEKTA YA MADINI:
Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa, yenye hazina kubwa ya madini mbalimbali. Madini yanayopatikana ni dhahabu, almasi, vito, madini ya viwandani kama chokaa, madini ya ujenzi kama vile kokoto, mawe ya nakshi na Mchanga. Aidha madini hayo yanapatikana katika Wilaya za Urambo, Uyui, Tabora Mjini, Nzega, Sikonge na Igunga. Maeneo ambayo tayari yanachimbwa madini ni Lusu – Nzega, ambako kuna Mgodi mkubwa wa dhahabu wa Kampuni ya Resolute (T) Ltd ambao katika kipindi cha mwaka 2007 ulisafirisha miche ya dhahabu yenye uzito wa Kgs 4,955.4 yenye thamani ya $ 98,186,310 ukilinganisha na Kgs 4,480:84 yenye thamani ya $ 82,141,568 iliyosafirishwa mwaka 2006. Matinje, Igurubi, Bulangamilwa, Buchenjegele (katika Wilaya ya Igunga) na Uyowa Wilayani Urambo ni maeneo yenye viwanja vya wachimbaji wadogo ambao wanaendelea na uzalishaji duni wa dhahabu. Uzalishaji duni unatokana na sababu ya kutokuwa na nyenzo za kisasa kwa ajili ya uchimbaji bora wenye tija. Mbogwe (Nzega) ni eneo lenye madini ya almasi ambapo kuna wachimbaji wadogo. Eneo hili limepata wabia wenye nia ya kuwasaidia wachimbaji hao waweze kuzalisha madini kwa njia bora zaidi. Itanana na Mahene katika Tarafa ya Bukene Wilayani Nzega ni maeneo ambayo yanafanyiwa utafiti wa kina na Kampuni ya Kimcor kwa ajili ya kuchimba almasi. Hivyo utafiti huu ni wakuchukua sampuli nyingi zaidi (Bulk sample) ili kuweza kuhakiki uzalishaji wa madini hayo katika eneo hilo . Taarifa za tafiti za awali katika maeneo hayo zinaonyesha kuna uwezekano mkubwa wa kufungua mgodi wa almasi. Wilayani Uyui kuna maeneo yanafanyiwa utafiti na Kampuni ya Savannah Exploration. Lengo ni kutafuta mashapo yenye mwamba wa Almasi (Kimberlite) kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo.
SHUGHULI ZA UTAFITI:Katika Mkoa wa Tabora kuna leseni 83 za utafiti wa awali na utafiti wa kina, watafiti hawa wanatafiti madini ya dhahabu na almasi. Yafuatayo ni Makampuni ambayo yanafanya kazi za utafiti katika Mkoa huu: Savannah Exploration Co.Ltd. (Almasi) Barrick Exploration Africa Ltd (Dhahabu) Resolute (T) Ltd (Dhahabu) Twing Gold Exploration Ltd (Dhahabu) Kimcor (Almasi) Katika Sekta ya madini Mkoa tunahamasisha uwekezaji wa uchimbaji na utafiti. Pili Makampuni ya wazalendo tunayakaribisha kuwekeza katika ununuzi wa dhahabu katika Mkoa wetu.
|
|
||||||||||||||||||||||||
| Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274 | ||