JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
     
 
     
AFYA
 
Afya [ Rudi nyumbani ] au
 
 
 

SEKTA YA AFYA

HUDUMA ZA AFYA (Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati):

Mnamo mwaka wa 2005, Mkoa wa Tabora ulikuwa na jumla ya vituo vya kutolea huduma kama ifuatavyo: Hospitali 7, Vituo vya Afya 18 na Zahanati 211. Mwaka 2009, Mkoa wa Tabora una jumla ya vituo vya kutolea huduma kama ifuatavyo: Hospitali 7, Vituo vya Afya 22 na Zahanati 227 kama inavyoonyeshwa katika jedwali Na.21. Kuna ongezeka la vituo vya Afya 3 sawa na asilimia 27, na Zahanati 7 (sawa na asilimia 4.1).

Watumishi:

Mkoa una watumishi 902 wanaotoa huduma, idadi ambayo ni chini ikilinganishwa na mahitaji kiasi cha watumishi 1,994. Upungufu ni watumishi 1,144, sawa na asilimia 57.3 ya mahitaji. Watumishi wa fani mbalimbali waliopo ni kama inavyoonyeshwa katika jedwali Na. 24 hapa chini:

 

Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund (HBF):

Mfuko wa Afya wa Pamoja (HBF) unahudumia shughuli za kawaida za Sekta ya Afya na miradi ya kuboresha utoaji wa huduma za Afya

kwa kuimarisha miundombinu kama Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali. Mpango wa HBF kwa Mkoa wa Tabora ulianza mwaka 2002, ambapo Wilaya za Tabora, Igunga na Uyui zilihusika. Kwa mwaka 2003, Wilaya za Nzega, Urambo na Sikonge nazo ziliingia katika Mpango huu.

Kupitia Mfuko huu, Mkoa ulipata kiasi cha Tshs. 660,882,175/= Mwaka 2005, Tshs.902,030,390/= mwaka 2006 Tshs.1,950,153,875/= mwaka 2007 na Tshs.2,459,506,000/= mwaka 2008/2009

Matokeo ya Mpango huu wa HBF ni kwamba mazingira ya utoaji huduma za afya yameendelea kuboreka, ukiachilia mbali upungufu mkubwa wa wahudumu wa vituo vya kutolea huduma.

Idadi ya vituo vya kutolea huduma nayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hali ambayo inaleta haja ya kuwa na mkakati wa kuongeza watumishi wa kutosha katika vituo Mkoani; kwa shabaha ya kuongeza ufanisi na ubora wa utoaji wa huduma za afya.

 

MRADI WAMFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF):

Mfuko wa Afya ya Jamii unalenga katika kuboresha afya za wananchi kwa kuwapatia huduma bora za matibabu na kuimarisha Vituo vya Afya na Zahanati na kutoa Elimu ya Afya na Kinga. Baada ya mafanikio ya Wilaya ya Igunga, Wilaya zingine nazo zimeanzisha CHF isipokuwa Wilaya ya Tabora

 

Magonjwa ya Mlipuko:

Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008, magonjwa matano ya mlipuko yaliyojitokeza hapa Mkoani.

Mkoa umeweza kudhibiti magonjwa ya mlipuko kutokana na elimu ya afya na mazingira inayotolewa kwa jamii kwa mfano:

•  Kata 12 kati ya Kata 4 zimejenga vyoo

•  Ukaguzi wa mazingira katika vyumba za makazi 55,936, taasisi 287 na vyumba vya biashara 467 umefanyika, ambako lengo lilikuwa ni ukaguzi vya vyumba vya makazi 20,105, taasisi 168 na vyumba vya biashara 100.

Kutokana na uthibiti huo Mkoa haukupata ugonjwa wa kipindupindu kwa kipindi hicho.

Uchafuzi wa mazingira nao umepungua kwa asilimia 14% ukilinganisha na lengo la Kitaifa la 20% hadi 10%. Hata hivyo jitihada za kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga vyoo bora na kuvitumia, zinaendelea.

Kuhusu kupunguza maji machafu yenye madhara yanayotoka viwandani na katika kilimo, Mkoa wa Tabora una viwanda vichache, hivyo uchafuzi wa maji ni mdogo ikilinganishwa na Mikoa yenye viwanda vingi.


HALI YA VITUO VYA HUDUMA ZA AFYA NA MPANGO WA AFYA YA MSINGI (MMAM):

 

Mkoa una jumla ya Vituo vya Afya 22, na Zahanati 227

Aidha katika kusogeza huduma ya afya kwa jamii kwa kila Kata kuwa

na Kituo cha Afya na kila kijiji kuwa na Zahanati, Serikali imeanzisha Mpango wa MMAM.

Utekelezaji wa mpango huu unafanyika kwa kila Wilaya kuhamasisha jamii kushiriki katika ujenzi wa zahanati kwenye vijiji (hasa vijiji visivyo na zahanati.

Aidha Wilaya zote zimepata michoro ya majengo ya zahanati hizo toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Vile vile vijiji vimeshachagua maeneo husika ya kujenga zahanati na vituo vya afya.

 

HALI YA AFYA YA UZAZI NA WATOTO:

Mkoa una idadi ya watoto 103,434 wenye umri wa miezi 0 – 11 na watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 – 5 ni 550,387 ambapo wanawake wa umri wa kuzaa ni 479,487.

Kwa mwaka 2008, jumla ya wanawake 50,759 walijifungua kati ya 103,434 waliotarajiwa kujifungua, sawa na asilimia 49.1. Wazazi waliojifungulia kwenye Vituo vya Tiba ni 42,584, sawa na asilimia 86 ya wazazi wote waliojifungua. Wazazi 6,134, sawa na asilimia 12 walijifungulia nyumbani kwa Wakunga wa Jadi (TBAs), ambapo wazazi 2,074 walijifungulia nyumbani, sawa na 4%.

Katika kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo vya watoto 95 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai hadi 50 mwaka 2010, Mkoa umeweza kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 95 hadi 45 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai. Mafanikio hayo yametokana na:

•  Kukarabati Zahanati 133

•  Kujenga Zahanati 79

•  Kukarabati Vituo vya Afya 17

•  Kujenga Vituo vya Afya 4

•  Kujenga Nyumba za Watumishi 60

•  Kuajiriwa kwa Wauguzi 91

•  Kuajiriwa kwa Madaktari 16

•  Kuajiriwa kwa Mafamasia 12

Mkoa umeweza kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka 5 kutoka vifo 154/1000 hadi vifo 81/1000. Mafanikio hayo yametokana na mwitikio mzuri kwa wananchi kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo.

Aidha Mkoa umeweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka vifo 529/100,000 hadi vifo 209/100,000 kutokana na:

•  Mafunzo ya huduma za wajawazito (FANC) na mafunzo ya kuokoa maisha ya akina mama wazazi (LSS) yanayotolewa kwa watoa huduma wanaofanya kazi kliniki na wodi za wazazi.

Kuhusu kiwango cha wazazi wanaozalishwa na wakunga waliopata mafunzo, kutoka lengo la 50% hadi 80%, Mkoa umefanikiwa kufikia 72%. Hii imetokana na kuongezeka kwa kutolewa kwa Elimu ya Afya ya Uzazi na Mtoto kwenye Vituo vya Huduma.

 

Mafanikio

•  Wazazi wengi wamejifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma kwa asilimia 86.

•  Ubora wa ukusanyaji wa takwimu za vifo vya wazazi umeongezeka kwani takwimu zinapatikana za kutosha katika ngazi ya jamii.

•  Benki ya damu salama ya kanda inaendelea kutoa huduma vizuri.

 

HALI YA MAAMBUKIZI YA VVU NA UKIMWI MKOANI TABORA:

Kuimarisha vita dhidi ya UKIMWI:

Ili kupunguza maambukizi ya VVU na Ukimwi, Mkoa umefanikiwa kupunguza kutoka asilimia 11 (mwaka 2003) hadi 6.4 mwaka huu. Mafanikio hayo yametokana na kutolewa kwa Elimu Juu ya VVU kwa vijana.

Katika eneo la walemavu (wanawake na wanaume wenye umri wa miaka 15 – 35,) maambukizo yamepungua kwa asilimia 1.

Unyanyapa dhidi ya watu wenye VVU umepungua kwa asilimia 45%. Hii ni kutokana na uhamasishaji katika Jamii.

 
         
 
Afya [ Rudi nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2008 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, S.L.P. 25, TABORA. TEL: 026 - 2604058/2604116, FAX: 026-2604274